Kamanda wa Polisi mkoani
Arusha, Liberatus Sabas, amesema tuhuma alizotoa Mbunge wa Arusha Mjini,
Godbless Lema (Chadema) kuwa jeshi lake linamwonea kwa kumkamata na kumuweka
mahabusu ovyo, wakati yeye sio mhalifu siyo za kweli na kwamba Mbunge huyo
(pichani) amekuwa chanzo cha vurugu katika uandikishwaji wa daftari la
wapigakura.
Sabas alisema jana kuwa Lema
anasababisha vurugu kwa kutembelea maeneo ambayo watu wamejitokeza na
kujiandikisha na kuhutubia, kitu ambacho ni kinyume cha sheria.
“Yeye kama anataka kuhamasisha watu
hatukatai, aende maeneo ambayo daftari bado halijafika akahamasishe na likifika
aache wananchi wajiandikishe na siyo kuwafuata kwenye mistari na kuanza kupiga
hatuba, siyo sahihi,” alisema.
Aliongeza: “Kwanini anapokuwapo Lema
vurugu zinatokea, asipokuwapo hakuna vurugu, yeye asiende kwa watu ambao tayari
wamejitokeza kujiandikisha, aende kwa ambao bado hawajafikiwa na daftari hilo.”
Sabas alisema kuwa Jeshi la polisi
haliwezi kuonea mtu wala yeye (Lema) isipokuwa likipata taarifa kama siku ya
tukio ya Juni 20 alipokamatwa kuwa analeta vurugu na wananchi hawataki kumwona
katika maeneo ya uandikishaji ndipo walipokwenda kumkamata.
Alisema siku ya tukio walipata
taarifa kutoka kwa askari walioko doria kwenye kituo cha Olsunyai kuwa kuna
vurugu zinazofanywa ma Mbunge huyo na kuomba ulinzi uongezwe na askari
wakapelekwa zaidi na kumtia mbaroni na wenzake 24 na aliyetoa taarifa polisi
aliomba ulinzi.
“Lakini pia Lema anaongozana na
kundi la watu toka maeneo tofauti ya uandikishaji, kitu ambacho siyo sahihi pia
nacho kinakera baadhi ya watu,” alisema.
Hata hivyo, alisema uchunguzi dhidi
ya tuhuma zake unaendelea na ukikamilika atachukuliwa hatua stahiki.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment