BVR yazua vurugu Zanzibar.
23:18 by Kwetuhouse Media
Uandikishaji wa Daftari la Wapigakura kwa mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR) katika maeneo ya wilaya ya Magharibi A, Zanzibar jana ulianza kwa dosari na kusababisha vurugu katika baadhi ya vituo.
Vurugu hizo zilitokana na sababu mbalimbali ikiwamo uchache wa vifaa vya uandikishaji na hamasa kubwa ya wananchi kutaka kujiandikisha.
Katika uandikishaji huo unaosimamiwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ni kuandikisha wapigakura ambao wana sifa za kuandikishwa ikiwamo umri wa miaka 18 kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu. Kutokana na vurugu hizo ikiwamo watu kupigana na kusukumana ili kupata fursa ya kujiandikisha, askari polisi na vikosi vingine vya ulinzi walimwagwa katika vituo mbalimbali ili kudhibiti uwezekano wa kupotea kwa amani.
Vurugu hizo pamoja na mambo mengine, zilisababishwa na wingi wa watu waliojitokeza na kusababisha changamoto kubwa kwa waandikishaji.
Baadhi ya vituo vilivyokumbwa na vurugu hizo ni Mtoni na Mtoni Kidatu katika wilaya hiyo huku wananchi wakilalamikia uchache wa BVR.
“Tupo hapa toka saa kumi na mbili asubuhi, lakini zoezi haliendi vizuri, tatizo lililopo ni uchache wa mashine, mashine moja tu ndio inayotumika na kama hali unavyoiona watu ni wengi sana,” alisema Asha Makame Haji katika kituo cha Mtoni.
Aidha, alisema idadi kubwa ya watu waliofika kujiandikisha ilitokana na baadhi yao kutokuwa wakazi wa eneo husika
Akizungumzia tatizo la uchache wa BVR, afisa wa uandikishaji wa kituo cha Mtoni, Chum Ali Abeid, alisema tayari wameshaagiza mashine nyingine ili kutatua tatizo hilo.
“Kweli watu ni wengi sana na wapo hapa toka asubuhi, lakini mashine tuliyonayo ni moja na tayari tumeshaagiza mashine nyingine,” alisema.
Msimamizi wa kituo cha uandikishaji cha Kibweni, Omar Ali Khamis, alisema uandikishaji unaendelea vizuri na wananchi hasa vijana wamehamasika kufika kujiandikisha, lakini changamoto zilizopo katika kituo hicho ni baadhi ya wananchi kuchanganya vituo vyao vya kujiandikisha na kwenda katika vituo ambavyo sio vinavyowahusu.
Afisa mmoja kutoka ZEC ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema mashine za BVR walizonazo zinatosheleza kwani uandikishaji katika kila wilaya utachukua siku nne na watu wote wataandikishwa na hakuna atakayenyimwa haki yake.
“Zoezi linaenda vizuri isipokuwa wananchi wana haraka, wanataka lazima wote waandikishwe siku moja wakati bado siku zipo za uandikishaji,” alisema afisa huyo.
0 comments:
Post a Comment