Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli,
ambaye ni miongoni mwa mawaziri 13 waliochukua fomu ya kuomba kuteuliwa
kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi
(CCM), jana alirejesha fomu hiyo kimya kimya huku akikwepa kuzungumzia safari
yake ya kusaka wadhamini katika mikoa 23 aliyopita.
Magufuli aliyechukua fomu hiyo Juni
5, mwaka huu, Makao Makuu ya CCM mjini Dodoma, zikiwa ni siku mbili tangu chama
hicho kifungue milango kwa wagombea urais kuchukua fomu.
Hata hivyo, Dk. Magufuli, hakuwahi
kutangaza nia wala kuzungumza na Watanzania kupitia vyombo vya habari kama
walivyofanya makada wenzake waliojitosa kutaka kumrithi Rais Jakaya Kikwete.
Tangu alipotangaza nia, Dk. Magufuli
hajawahi kueleza vipaumbele vyake iwapo atateuliwa na chama chake kugombea kiti
hicho, wala kujinasibu kama wagombea wenzake wanavyofanya kila mkoa waliopita
kusaka wadhamini na kisha kupewa fursa ya kuzungumza na wanachama wa CCM na wananchi
kwa ujumla. Akiwa Makao Makuu ya CCM mjini hapa, Waziri Magufuli alikabidhi
fomu yake kwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Rajab Luhwavi, saa 4:10 asubuhi
ikiwa na wadhamini 450 pekee.
Akikabidhi fomu hiyo, Waziri
Magufuli alisema: “Nimezunguka katika mikoa 23 ya nchi hii na nimepata
wadhamini kwenye mikoa 15, kikanuni inapaswa kuwa hivyo lakini nina ziada ya
wadhamini kutoka mikoa ya Tabora, Geita, Mwanza, Kilimanjaro, Mtwara, Mara,
Iringa, Pemba na Unguja. Mkitaka niwakabidhi pia kuonyesha ninavyokubalika
nitawapa,” alisema na kuongeza: “Mheshimiwa huko kote nilikokwenda nilikuwa
natumia ramani ambayo inaonyesha nimepita wapi na wapi? Nimekuja nayo naomba
nikukabidhi Mheshimiwa Naibu Katibu Mkuu Bara.” Alipomaliza aligoma kuzungumza
na vyombo vya habari na kuondoka.
WASIRA
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika, Steven Wasira, ambaye naye alirejesha fomu hiyo saa 7:47
mchana, akiwa amesindikizwa na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka na
Mbunge wa Tarime (CCM), Nyambari Nyangwine alisema:
“Kama mnavyotuona na wenzangu hapa,
afya yangu ni nzuri na haina taabu, nimefanya majaribio ya kutembea nchi nzima
kuona kama afya yangu iko safi. Nasubiri nikiteuliwa na kuingia kwenye mshike
mshike wa siku 90 za kampeni za uchaguzi mkuu, nitawachezesha ‘kwata’ hao
wanaojiita Ukawa (Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi) hadi
tutakapoachana njia ya kwenda Ikulu.”
Wasira alipoulizwa iwapo anaweza
kuwapiku wagombea wenzake ambao wanapewa nafasi kubwa ya kuteuliwa, alisema
amewaomba Watanzania huko alikopita wafunge kwa sala na kumuombea atinge katika
hatua ya tano bora, tatu bora na kisha awe mteule wa CCM atakayepeperusha
bendera katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
KIGWANGALLA: KIZAZI CHA VIJANA,
WAZEE WASHAURI
Mgombea mwingine wa urais
kupitia (CCM), Dk. Khamis Kigwangalla, amewaeleza wanachama wa chama
hicho kuwa Taifa linahitaji viongozi vijana katika kuongoza nchi, huku nafasi
ya wazee ikibaki kwenye kushaurina na kutoa maelekezo pale watakapobaini kuna
tatizo.
Dk. Kigwangalla alitoa kauli hiyo
jana mjini Lindi alipokuwa akizungumza na wanachama waliokuwa wamejitokeza
kumdhamini katika kinyang’anyiro hicho kinachotarajia kukamilika Julai 12,
mwaka huu kupitia CCM.
Akizungumza na wanachama wa CCM
Makao Makuu ya chama hicho mkoani Lindi, Dk. Kigwangalla alisema ameamua kuomba
nafasi hiyo akisema anajiamini na anayo maarifa ya kutosha katika kuliongoza
Taifa iwapo atapewa ridhaa hiyo.
Dk. Kigwangalla ambaye pia ni Mbunge
wa Nzega, alisema anazifahamu changamoto mbalimbali zinazowakabili Watanzania
zikiwamo masuala mazima ya dunia ya leo pamoja na ya kupata ukombozi.
Aidha, alipinga madai yanayotolewa
na baadhi ya watu kwamba vijana hawastahili kushika madaraka hayo ya juu
yakiwamo ya urais, hayana msingi kwani wazee tayari wamefanya kazi kubwa
ikiwamo kuwasomesha na kupigania uhuru wa nchi yao.
“Hivi sasa kumekuwa na maeneo mengi
yanasemwa kuhusiana na uzoefu na uongozi…watu wengine wanasema vijana wadogo
sana wana haraka ya kutaka madaraka makubwa tofauti na umri walionao,” alisema
Dk. Kigwangalla.
Dk. Kigwangalla alisema wakati
umefika kwa wazee wakapumzika kutokana na kazi kubwa waliyoifanya na kuiachia
fursa hiyo kwa vijana ambao wana nguvu za kutosha na chachu ya kuliletea Taifa
maendeleo.
Alisema iwapo Chama kitampa tiketi
na Watanzania wakampatia ridhaa, atahakikisha serikali atakayoiunda ndani yake
mnakuwa na wazee kwa ajili ya kusaidia ushauri pamoja na kuwapa kumbukumbu ya
mambo yaliyokuwa yanafanyika siku za nyuma.
Kwa mujibu wa Dk. Kigwangalla, zama
za wazee kuongoza Taifa zilianza wakati wanapigania Uhuru wa Taifa nao hawakuwa
ni wazee bali vijana.
“Mawaziri wote wa serikali ya awamu
ya kwanza ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, miaka ile ya 60
tulipokuwa tunapata Uhuru wetu, walikuwa vijana kati ya umri wa miaka 25 na
kuendelea na ndiyo hao hao mpaka leo wanaendelea kuwapo,” alisema Dk.
Kigwangalla.
Alifafanua kuwa matamshi
yanayotolewa na baadhi ya watangaza nia kuwa wao ndiyo wenye uwezo na sifa ya
kuliongoza Taifa, hayana msingi kwani wote wanaoiomba nafasi hiyo hakuna
aliyekwisha ifanya.
“Nafasi hii tunayoiomba kwenu hivi
sasa kama ningekuwa nagombea na wazee kama vile mzee Mwinyi, Mkapa na sasa
Kikwete anayemaliza muda wake, nisingekuwa na ubishi kwani ndiyo wenye uzoefu
kwani wamepitia kazi hiyo ya urais,” alisema Dk. Kigwangalla. Dk. Kigwangalla
alipata wadamini 35 mkoani Lindi.
MWINGINE ACHUKUA FOMU
Katika hatua nyingine, Ofisa
Maendeleo ya Jamii, Ritha Peter Ngowi (50), mkazi wa Kilimanjaro na Dar es Salaam,
amekuwa mwanamke wa tano kutangaza nia ya kuomba kuteuliwa na CCM kugombea
urais akieleza iwapo chama chake kitamteua na kisha Watanzania kumpa ridhaa;
atahakikisha anatenga kambi maalum itakayowaweka pamoja watu wenye ulemavu na
wengine wenye hali inayofanana na hiyo ili kuwapa ujuzi utakaowahakikishia
uhakika wa kuwa na kipato kwa maisha yao yote.
Wanawake wengine waliojitosa
kugombea kiti hicho ni Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro; Naibu
Waziri wa zamani wa Fedha na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Monica Mbega; Balozi
Amina Salum Ali na Dk. Mwele Malecela.
"...nikiwa Rais, sitaki
awapo Mtanzania yeyote ambaye hana kipato cha kumwezesha kuishi na kwa kuanzia
nataka kila Mtanzania apate elimu stahiki,” alisema Ritha.
Mgombea huyo alisema iwapo CCM
itampa ridhaa na Watanzania kumuamini na kumchagua kuwa Rais wao, atahakikisha
kwamba wafanyakazi wa serikali na taasisi za umma wanakuwa na mishahara minono
ambayo itawawezesha kuishi bila ya kutegemea hisani wala mikopo ambayo
hukwangua miamala yao ya kibenki katika taasisi za fedha.
BALOZI KARUME
Balozi Ali Karume, jana alirejesha
fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea urais huku akieleza kuwa kutokana na
changamoto alizokutana nazo katika safari ya kusaka wadhamini; akichaguliwa
kupeperusha bendera ya chama
chake na baadaye Watanzania wakampa
ridhaa ya kwenda Ikulu, atachukua uamuzi mgumu wa kupunguza kodi zinazowanyonga
wananchi wa kawaida.
“Nikiwa Rais, nitapunguza kodi
zinazowanyonga wananchi wa chini; lengo langu ni kulipeleka taifa kwenye uchumi
wa kati na kuiacha nchi kwenye amani na utulivu. Ni lazima katika utawala wangu
niutetee kwa nguvu zote Muungano,” alisema Balozi Karume.
Karume ambaye ni mwanadiplomasia,
alimkabidhi fomu hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Rajab Luhwavi, saa
10:28 jioni, Makao Makuu ya CCM mjini Dodoma baada ya kuzunguka mikoa yote ya
Zanzibar na mikoa kadhaa ya Tanzania Bara.
Baada ya kukabidhi fomu hiyo; Karume
alisita kuitaja idadi ya mikoa aliyopita kusaka wadhamini wake, akisema:
“Nimezunguka mikoa yote ya Bara lakini hampaswi kujua, isipokuwa nimepita mikoa
ya kutosha. Itoshe kusema tu kwamba nimekuwa mgombea wa sita kurejesha fomu na
mgombea wa nane kuchukua fomu Juni 4, mwaka huu…Nimepata wadhamin 450 tu na
wengine waliojitokeza kunidhamini niliwaacha na kuwaomba radhi,” alisema Balozi
Karume.
Mbio za kugombea urais hazikuanza
leo kwa Balozi Karume, kwa kuwa mwaka 2000 alitangaza nia na kuingia katika
kinyang’anyiro cha uteuzi ndani ya CCM kwa upande wa Rais wa Zanzibar, lakini
alijitoa katika hatua za awali na kumuachia nduguye, Amani Abeid Karume.
Mwaka 2005 na mwaka 2010, alijitosa
katika kugombea uteuzi wa chama chake ili apeperushe bendera ya CCM kwa urais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini pia bahati haikuwa yake.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment