Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiifungua Semina ya Siku moja
juu ya mwenendo wa sarafu ya Tanzania dhidi ya Dola ya Kimarekani kwa
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Hapo Ukumbi wa Baraza hilo Mbweni Nje
kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba thamani
ya shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Kimarekani huathirika mara kwa
mara kutokana na Taifa kutegemea kuagiza bidhaa zaidi kutoka nje badala
ya bidhaa hizo kuzalishwa na makampuni ya hapa nchini
Alisema
nyingi ya biadhaa zinazoingizwa Nchini huagizwa kwa fedha za kigeni,
hususan Dola za Kimarekani na kuuzwa kwa fedha za Kitanzania jambo
ambalo hushajiisha uingizaji zaidi wa bidhaa na huduma kutoka nje.
Balozi
Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akiifungua Semina ya siku moja ya
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi juu ya mwenendo wa Sarafu ya Tanzania
dhidi ya Dola ya Marekani iliyofanyika katika Ukumbi wa juu wa Baraza la
Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Alisema
athari ya kuteremka kwa thamani ya sarafu ya Shilingi ya Tanzania hasa
katika kipindi cha hivi karibuni imekuwa kubwa zaidi kuliko faida yake
na kupelekea kuzuka kwa malalamiko kwa Wananchi waliowengi hasa
wafanyabiashara kutokana na kubadilika sana kiwango cha sarafu hiyo
dhidi ya Dola.
Balozi
Seif alieleza kwamba kiwango cha ubadilishaji wa fedha kimekuwa ni
mojawapo ya kubebea mfuko wa bei nchini ikishuhudiwa kupanda kwa bei za
bidhaa zikiwemo zile zinazotengenezwa hapa nchini ikitwaja sababu kubwa
ni mwenendo wa thamani ya shilingi dhidi ya dola.
“
Hivi karibuni tumeshuhudia kupanda kwa bei za bidhaa, zikikwemo
zinazotengenezwa na kuzalishwa humu humu nchini sababu inayotajwakuwa
ni mwenendo wa thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya Kimarekani “.
Alisema Balozi Seif.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar alishauri kwamba ili kukabiliana na
changamoto hiyo ya kuyumba kwa Thamani ya Shilingi ya Kitanzania umefika
wakati kwa Wafanyabiashara na wawekezaji wa sekta ya Viwanda wajitahidi
kuongeza uzalishaji kwa kutumia rasilmali za ndani ili kudhibiti mfumko
huo.
Mapema
Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Bwana Juma Hassan Reli alisema
Fedha za Kigeni ziliadimika Nchini Tanzania katika miaka ya 80 kutokana
na udhibiti wa fedha hizo kusimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania chini ya
Sheria ya kudhibiti fedha za kigeni ya mwaka 1965.
Bwana
Juma Reli alisema hali hiyo ilifungua mianya ya rushwa hasa kwa wale
waliopewa dhamana ya kusimamia upatikanaji wa fedha za kigeni kwa bei
rasmi ambayo katika miaka ya kati ya 1967 - 1984 Dola moja ya Kimarekani
ilibadilishwa kati ya shilingi 7.14 hadi shilingi 8.13 za Kitanzania.
Alisema
mfumo huo pia ulichochea utoroshwaji wa mitaji kupelekwa nje ya nchi
kwani Watanzani walio wengi wakipata fedha za kigeni kwa kutumia njia
mbali mbali walishawishika kuzitunza fedha hizo katika Mabenki ya nje ya
nchi ili kukwepa sheria.
Ili
kuondokana na changamoto hizo Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania
alieleza kwamba Serikali ilifanya mageuzi kupitia sheria ya fedha za
Kigeni iliyopitishwa na Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya
mwaka 1992 ambayo inamruhusu mtu yeyote kumiliki kiasi chochote cha
fedha za kigeni au dhahabu ghafi hapa Nchini.
Alisema
Wananchi hivi sasa wana haki ya kununua na kuuza fedha za kigeni kwenye
maduka ya kubadilishia fedha pamoja na kuwa na akaunti ya fedha hizo
katika mabenki ya Biashara, jukumu la Benki Kuu likibakia kuhakikisha
kuwa soko la fedha linaanzishwa na kuendeshwa kwa nguvu za soko.
Bwana
Reli alifafanua wazi kwamba soko liliopo sasa la fedha za kigeni
linaendelea kukua ambapo ndio msingi mkuu wa kuweka thamani ya shilingi
ya Tanzania baada ya kuanzishwa na Benki Kuu ya Tanzania mwaka 1994.
Akitoa
Mada kwenye Semina juu ya mwenendo wa Sarafu ya Tanzania dhidi ya Dola
ya Marekani Mkurugenzi wa Sera za Kiuchumi na Utafiti wa Benki Kuu ya
Tanzania Dr. Masawe Joseph alisema sarafu ya Fedha ya Tanzania imeachwa
kwenye soko ili kuiwezesha iende sambamba na masoko mengine ya Sarafu
Ulimwenguni.
Dr.
Masawe alisema mwenendo wa Shilingi ya Tanzania imeshuka thamani na
kuufanya mfumko wa Bei Nchini kufikia asilimia 5.4% ikilinganishwa na
Mataifa mengine Duniani zikiwemo baadhi ya Nchi za Bara la Afrika ambazo
mfumko wao uko chini ya asilimia 3%.
Mkurugenzi
wa Sera za Kiuchumi na Utafiti wa Benki Kuu ya Tanzania
alifafanua kwamba upungufu wa mapato yanayotokana na bidhaa ya dhahabu
na bidhaa nyengine asilia umefidiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na
kuongezeka kwa bidhaa za viwanda zinazozalishwa na kusafirishwa nje ya
Nchi.
Alisema
fidia hiyo imeifanya sekta ya Viwanda kukua na kukusanya mapato ya
zaidi ya Dola za Kimarekani Elfu Moja kwa sasa kutoka Dola Mia Nane
mwaka uliopita ikitanguliwa na Sekta ya Utalii ambayo kwa sasa
inashikilia nambari Moja katika kuchangia pato la Taifa.
“Lazima
tuangalie hiyo shilingi ilipo kwa wakati husika ni mahala pake pazuri
bila ya kuathiri pande zote zinazohusika kati ya wakusanyaji, wauzaji na
watumiaji “. Alifafanua Mkurugenzi huyo wa Sera za Kiuchumi na Utafiti
wa Benki Kuu ya Tanzania.
Dr.
Masawe alieleza kwamba ni vyema ukawepo uwiano baina ya kushuka na
kupanda kwa sarafu ya shilingi kwa vile pande zote husika zina hasara na
kunufaika pia, lakini cha kuzingatia zaidi ni udhibiti makini wa mambo
hayo ya kupanda na kushuka.
Wakichangia
mada ya mwenendo wa thamani ya shilingi ya Tanzania iliyotolewa na
Mkurugenzi wa Sera za Kiuchumi na Utafiti wa Benki Kuu ya Tanzania Dr.
Masawe Joseph, baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walisema
uchumi wa Zanzibar unastahiki kuangaliwa kwa makini kulingana na
mazingira yake ili kujieusha na matatizo yanayotokana na kushuka kwa
sarafu ya Tanzania.
Wajumbe
hao walisema mazingira ya Zanzibar yanategemea uchumi wa bidhaa chache
ikilinganishwa na ule wa Tanzania Bara kiasi kwamba maisha ya wananchi
walio wengi Visiwani yanategemea Kilimo ambacho bado hakijawa na nguvu
za kuwafanya wawe na uwezo wa kusafirisha kwa lengo la kupata uchumi
imara.
Waliushauri
Uongozi wa Benki Kuu ya Tanzania kuyaangalia mashirikia na Taasisi za
Kiuchumi Nchini katika kuziwezesha wakati inapotokea hali au mazingira
ya kuporomoka kwa sarafu ya shilingi ya Tanzania kwenye soko la Dunia.
Walifahamisha
kwamba yao mashirika na Taasisi zisizopungua 90 Tanzania Bara ambazo
ziliwahi kupewa nguvu ya uwezeshaji na Benki Kuu ya Tanzania katika
kujiendesha wakati wa kuporomoka kwa soko la Sarafu
Ulimwenguni miaka michache iliyoita.
Walieleza
kwamba uimarishaji wa Mashirika na Taasisi za ndani ya Nchi utaongeza
ufanisi sambamba na kuwapunguzia ukali wa maisha wafanyakazi wa Taasisi
za umma na hata binafsi ambao ndani ya miezi mitatu iliyopita
wameshindwa kukidhi mahitaji yao kutokana na kushuka kwa thamani ya
shilingi.
Wawakilishi
hao wameishauri Benki Kuu ya Tanzania kuangalia mazingira ya matumizi
ya fedha ya kigeni kama Yuan ya Jamuhuri ya Watu wa china kutokana na
wafanyabiasha wengi wa Tanzania kwa zaidi ya asilimia 75% kuendesha
biashara zao katika soko la China.
Naibu
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Bwana Juma Hassan Reli akitoa ufafanuzi
kabla ya kuanza kwa semina ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar
juu ya mwenendo wa sarafu ya Tanzania dhidi ya Dola ya Kimarekani.
Mkurugenzi
wa Sera za Kiuchumi na Utafiti wa Benki Kuu ya Tanzania Dr. Masawe
Joseph akitoa Mada kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi juu ya mwenendo
wa sarafu ya Tanzania.
Spika
wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Pandu Ameir Kificho wa pili
kutoka kushoto akichangia pamoja na kuliza maswali kwenye semina ya
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar juu ya mwenendo wa sarafu ya
Tanzania dhidi ya Dola ya Kimarekani.
Wa
mwanzo kulia ya Spika Kificho ni Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi
Zanzibar Mh. Ali Abdulla Ali, kushoto ya Spika Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania
Bwana Juma Hassan Reli.
Baadhi
ya Watendaji wa Benki Kuu ya Tanzania {BOT} pamoja na Wajumbe wa Baraza
la Wawakilishi wakifuatilia michango na maswali mbali mbali yaliyokuwa
yakiulizwa na baadhi ya Wajumbe hao kwenye kwenye semina hiyo.
0 comments:
Post a Comment