Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji amesema atajiuzulu
wadhifa wa uenyekiti iwapo itabainika kuwa kweli yeye ni fisadi, mwizi na
muongo kama ambavyo Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi
amekuwa akisukuma mashambulizi dhidi yake.
Manji amezungumza na waandishi wa habari kwenye
makao makuu ya Yanga, leo na kueleza hayo huku akisisitiza kumtaka Mengi
ajitokeze na wakutane kwa ajili ya kufanya mdahalo wa wazi ambao utadhibitisha
kuhusiana na tuhuma hizo.
Alisema kuendelea kuiongoza Yanga wakati
imethibitika ni fisadi na mwizi, ni utovu wa nidhamu na wanachama wa klabu hiyo
watamtilia shaka.
Bilionea huyo ameyasema hayo leo Jumapili, mbele ya
wanachama wa klabu hiyo kwenye mkutano uliofanyika Makao Makuu ya Yanga,
makutano ya Mitaa ya Jangwani na Twiga jijini Dar.
Manji alifunguka kuwa Mengi amekuwa akimsakama kwa
muda mrefu na sasa amesema amechoka.
Manji anadai kilichomchefua zaidi ni habari
iliyotoka kwenye Gazeti la Nipashe kuwa kampuni yake ya Farm Equip Tanzania and
Quality Garage, ijulikanayo kama QG Engineering ilishindwa kulipa kiasi cha
bilioni 9.055 serikalini.
Manji amekanusha taarifa hiyo na kuomba Julai 3,
mwaka huu kukutana na mmiliki wa gazeti hilo, Mengi kwenye mdahalo ‘live’ na
kila upande uje na ushahidi wa kutosha kisha Watanzania wapige kura ili muongo
na mkweli ajulikane kuliko kuchafuliwa jina.
“Iwapo itabainika kweli mimi ni fisadi, muongo na
mwizi, niko tayari kuachi ngazi ya uenyekiti wa Yanga na sitagombea cheo
chochote hapa, maana klabu itakuwa inaongozwa na mtu asiye na vigezo sitahiki
vya kuwa kiongozi,” alisema Manji.
“Watu wanapaswa kujiuliza, mimi ni fisadi
ninayejulikana na vyombo vya habari vya IPP tu? Wengine hawaoni hilo? Je, kwa
nini IPP pekee ndiyo waone mimi ni fisadi? hapo watu wajiulize,” alisema Manji.
0 comments:
Post a Comment