Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya
Habari Tanzania (Moat) na wadau wengine, wamepinga Muswada wa Sheria ya
Upatikanaji wa Habari ya mwaka 2015, kupelekwa bungeni kwa kuwa unakiuka sheria
za kimataifa, katiba ya nchi na kuwanyima haki raia kupata taarifa na kuua
ndoto ya vijana wanaotarajia kunufaika na tasnia ya habari.
Wadau wengine waliopinga muswada huo
ni Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),
Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa) Tawi la Tanzania na
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu ( THRDC).
Akizungumza katika mkutano wa
Moat na wadau wa tasnia hiyo jana jijini Dar es Salaam, Mmiliki wa
Kampuni ya New Habari Cooperation, Rostam Aziz, alisema, muswada huo ni mbaya
kwani unazuia dhana nzima ya uwazi na ukweli hivyo kulirudisha taifa
nyuma.
Aliitaka serikali kusitisha
kuwasilisha uwasilishaji wa muswada huo bungeni hadi wadau wote wa tasnia ya
habari nchini watakapotoa maoni yao.
“Huu muswada ni mbaya…wala
hakuna haja ya kuwa na ‘debate’ (mjadala). Tuisihi serikali, isitishe kupeleka
muswada huu bungeni maana ni mbaya na utazaa ‘bad laws’ (sheria mbaya),”
alisema na kuongeza:
" Serikali isifanye haraka,
muswada huu unataturudisha nyuma kama taifa. Usitishwe kupelekwa bungeni hadi
pale wadau wote watakapotoa maoni yao, ” alisema Rostam.
Akitanganza maazimio hayo,
Mwenyekiti wa Moat, Dk. Reginald Mengi, alisema kupitishwa kwa muswada
huo kutawanyima uhuru wa usambazaji wa habari kwa vyombo vinavyomilikiwa na
watu binafsi jambo ambalo ni kinyume cha katiba ya nchi.
Dk. Mengi alieleza kushangazwa
na utungwaji wa sheria hiyo ambayo kwa upande mmoja inatambua na kuheshimu
misingi ya katiba katika ibara ya 5 na upande mwingine ibara ya 18 ikikataza
taarifa iliyotolewa chini ya ibara ya 5 (1) kwa umma na kutoa vitisho kwa
atakayekiuka na kupatikana na hatia ya kufungwa kifungo cha miaka isiyopungua
mitano jela.
“Huu ni mkanganyiko usioeleweka.
Upeo wa serikali hii, kwa maoni yangu ni kujaribu kuzima uhuru wa
kukusanya na kusambaza habari kwa wananchi. Ni mfumo na utaratibu wa hatari
kabisa kwa taifa letu,” alisema Dk. Mengi na kusisitiza kuwa:
“ Sielewi serikali inajaribu kufanya
nini hasa, kwa sababu hata chini ya mfumo wa chama kimoja ambao uliendelea hadi
mwanzoni mwa mwaka 1992, uhuru wa kutoa habari ulikuwapo na Tanzania ilikuwa
tayari imeruhusu magazeti binafsi kufanya kazi.”
Alisema uhuru wa kidemokrasia ni
nguzo muhimu kujenga taifa la amani na mshikamano na kwamba bila wananchi
kupata taarifa na habari za uhakika na za kweli, taifa litaweza kupoteza
heshima na utulivu wake.
Alihadharisha kuwa muswada huo
ukipitishwa, hakuna chombo cha habari cha binafsi kitakachokuwapo hivyo
kuua ndoto za vijana waliokuwa wanatarajia kunufaika na tasnia hiyo.
“Muswada ukipitishwa, hakuna
chombo chochote cha habari cha binafsi kitakachokuwapo, siyo redio wala TV
(televisheni). Ikitekelezwa ndiyo mwisho wa vyombo binafsi. Itamfanya kila mtu
atakayefanya kazi kwa uaminifu, kufungwa,” alisema Dk. Mengi.
Naye Mtaalamu wa Sheria, Damas
Ndumbaro, alisema utungwaji wa sheria unazingatia viwango vya kimataifa, katiba
ya nchi na haki za binadamu lakini baadhi ya vifungu katika muswada huo
vimekuwa kikwazo kwa waandishi wakiwamo wa habari za uchunguzi kwa kutakiwa
kutoa taarifa ndani ya siku 30 baada ya kupitia mamlaka husika.
“Haki ya kupata habari ni ya
kikatiba. Muswada huu una malengo manne, kutoa haki ya kupata taarifa,
kupromote transparency (uwazi), kupromote accountability (uwajibikaji) na
kuratibu masuala mengine yanayohusu habari. Je, malengo hayo
yamefanikiwa?" Alihoji.
"Sheria hii ikipita,
hakutakuwa na habari za uchunguzi (investigative journalism) tena,”
alisema.
Alisema muswada huo usiwe na jinai
za kutisha, ushirikishwe kwa wananchi kabla ya kutolewa na kuishauri
serikali kuchukua maoni ya wadau na kuyafanyia kazi.
MCT WAPINGA
Nalo Baraza la Habari Nchini (MCT),
limeiomba Kamati ya kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii ya Bunge
kumshauri Spika Anna Makinda asitishe kusomwa kwa muswada huo bungeni Juni 27,
mwaka huu.
Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi
Mukajanga, alisema baraza hilo limetoa ombi hilo kwa sababu wadau wa habari
hawakuwa na muda wa kutosha kutoa maoni yao baada ya kusomwa kwa mara ya kwanza
wiki iliyopita.
"Sisi kama wadau tumeiomba
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, imshauri Spika kwamba hakuna
muda wa kutosha, muswada huo usisomwe kwa mara ya pili na tatu katika mkutano
unaoendelea, uahirishwe uweze kufanyiwa kazi, mashauriano kati ya wadau na
serikali ili kuwa na andiko litakalokidhi vigezo na matakwa," alisema
Kajubi.
Alisema matarajio ya wadau ni
kuona serikali inayafanyia kazi maoni yao na muswada kwenda Kamati ya Kudumu ya
Katiba na Sheria ambayo itatazama na kumshauri Spika wa Bunge.
THRDC: MUSWADA UNAMINYA HAKI
Mwakilishi wa THRDC, Mariagoreth
Charles, amesema kipengele cha 18 kinakataza mpata taarifa kutosambaza taarifa
na hivyo kuminya haki ya kutoa taarifa na kusambaza kwa maslahi ya umma.
JUKATA: UTUNGWAJI SHERIA NI LAZIMA
USHIRIKISHE WADAU
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Jukata, Deus Kibamba, alisema katika muswada huo ni vifungu viwili pekee vyenye
unafuu na iwapo utapita, waandishi wengi watafungwa jela kwa makosa mbalimbali
ya kuhabarisha umma.
"Msingi wa kutunga sheria ni
kushirikisha wadau wote. Badala ya kuwa muswada wa kuwezesha upatikanaji huru
wa habari kwa wananchi, umekuwa wa kubana taarifa na kuleta vitisho kwa
wanaosaka na kusambaza taarifa. Mwandishi anaweza kwenda jela miaka 15 kwa
kufanya kitu ambacho sisi tunaona siyo kosa na hakuna mbadala wa faini,"
alisema.
TEF: MUSWADA HAUWEZI KWENDA POPOTE
Katibu Mtendaji wa Jukwaa la
Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena amesema muswada huo hauwezi kwenda
kokote na kama serikali itaendelea nao itakuwa haijashirikisha wadau na
hakutakuwa na sababu ya kuwaita watoe maoni.
Kwa mujibu wa Meena, kikao
hicho kilihudhuriwa pia na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo na Katibu
Mkuu wake, maofisa wa Idara ya Habari Maelezo, wote maofisa kutoka
Wizara ya Katiba na Sheria na mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, ambao
walisikia maoni ya wadau kuwa muswada huo haufai.
Mjumbe wa TEF, Jesse Kwayu,
alisema nyakati wanazoishi kwa sasa siyo za mabavu na serikali haiwezi kwenda
kwa namna hiyo kwani inapimwa katika vigezo vya utawala bora, uwazi na
ushirikishwaji kwa umma vinginevyo itajiwekea rekodi mbaya.
"Huu ni mchakato, unaweza
kutunga sheria leo, kesho ukasema ni mbovu na kuipigia kelele, sisi hatuchoki.
Ni imani yetu baada ya kuwaambia tuliyowaambia leo, hatuoni serikali ikiwa na
nguvu ya kusonga mbele na muswada huu kwa sababu haukidhi haja," alisema.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment