SERIKALI YASEMA UCHAGUZI UTAKUWA WA HURU NA HAKI NA UANDIKISHAJI WA WAPIGA KURA UNAKWENDA VIZURI

19:09 by Kwetuhouse Media



SERIKALI imesema Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu hautaahirishwa na kuvionya vyama vya upinzani visitumie suala la uandikishaji wa wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kuwatia hofu kwamba hautafanyika na kutumia kama mtaji wa kusababisha vurugu.

Akichangia hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016 bungeni mjini hapa jana kwa kujibu baadhi ya hoja zilizojitokeza wakati wa mjadala, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama, alisema uchaguzi upo palepale na kwamba uandikishaji wa wapigakura unakwenda vizuri na sasa bado mikoa ya Tanga, Pwani, Dar es Salaam na Zanzibar.

Waziri Mhagama alisema inashangaza baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wanawatia hofu wananchi kwamba uandikishaji huo utakwama na hakutakuwa na uchaguzi na kusisitiza kuwa Serikali haitavumilia jambo hilo na wanaofanya hivyo watashughulikiwa.

Alisema CCM haina mpango wa kuahirisha uchaguzi huo na imejipanga kwa kila hali, hivyo maoni ya wapinzani kwamba CCM inataka kuahirisha uchaguzi hayana ukweli wowote kwani Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete imefanya mambo makubwa zaidi ambayo wananchi wanayaelewa.

Alisema uandikishaji wapiga kura kwa mfumo wa BVR unakwenda vizuri, ambapo hivi sasa mikoa 10 imeanza uandikishaji wakati mikoa ambayo bado haijafanyika ni minne na wana uhakika muda si mrefu mikoa yote itakuwa imemalizika.

Naye Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba akichangia mjadala huo alisema ukiona zaidi ya watu 35 mpaka 40 katika chama kimoja wanaomba urais, hiyo ni dalili kwamba chama hicho kinakubalika na Rais atatokana na chama hicho.

Alisema hivi sasa mijadala katika sehemu mbalimbali ni kuhusiana na viongozi waliochukua fomu kuomba urais kupitia CCM akiwemo yeye jambo linalothibitisha kuwa CCM ni gari la uhakika na lazima Rais atatoka katika chama hicho.

“Hivi sasa mijadala kote ni kuhusu CCM, na kuhakikishia Mheshimiwa Mbowe (Freeman Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa Chadema, tukijaaliwa Oktoba utashuhudia Rais akitoka CCM na nitakuwa mimi na suti yangu nazindua Bunge,” alisema Nchemba na kuibua makofi na vicheko kwa wabunge.

Pia alisema serikali imeongeza umakini katika kusimamia deni la Taifa na imechukua hatua ya kuongeza uwezo wa kujitegemea katika makusanyo ya ndani.

0 comments:

Post a Comment