NEC yatishia kusitisha uandikishaji wa BVR.

19:19 by Kwetuhouse Media


Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetishia kuwa ikiwa viongozi wa kisiasa wataendelea kuingilia uandikishaji wa wapigakura kwa mfumo wa kielektroniki wa Biometric Voters Registration (BVR) haitasita kusitisha uandikishaji huo.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, alitoa tishio hilo wakati akizungumza na wadau mbalimbali wilayami Kilomnero, Morogoro baada ya kuhakiki mipaka ya jimbo jipya la Ifakara litakalomegwa kutoka Kilombero.

Alisema hivi karibuni imezuka tabia za viongozi wa kisiasa kuingilia kazi ya tume hiyo katika uandikishaji wa BVR na kusababisha fujo katika vituo vya uandikishaji na kwamba hawatavumilia tena kuona mambo hayo yakiendelea.

Alitolea mfano mkoani Arusha akisema wapo baadhi ya viongozi wa kisiasa wanajifanya wana haki ya kuingilia kazi hiyo na kusababisha fujo na kusema kuwa vifaa vinavyotumia mkoani humo ndivyo vilivyotumika katika mikoa mingine na hakuna malalamiko kama hayo na kuhoji kwa nini mkoa huo unakuwa tatizo.

Hata hivyo, alisema tayari wamepekeka mashine nyingine 10, lakini bado anashangaa viongozi hao wanalalamika na kuahidi kuwa wale wote wanaopaswa kuandikishwa lazima NEC itahakikisha wanaandikishwa hata kwa kuongeza siku na sio kuingiliwa kazi na wanasiasa.

0 comments:

Post a Comment