Serikali
imeshauriwa kununua helikopta (Chopa) katika kila mkoa kwa ajili ya kufanya
shughuli za zimamoto badala ya kutumia magari ambayo hayafiki kwa wakati katika
maeneo ya matukio kutokana na msongamano wa magari barabarani.
Ushauri
huo ulitolewa jana bungeni na Mbunge wa Mji Mkongwe (CUF), Muhammad Ibrahim
Sanya, alipokuwa akiuliza swali la nyongeza.
Katika
swali lake, mbunge huyo alihoji kwanini serikali isiwe na utaratibu wa kununua
Chopa kwa ajili ya kuwezesha vikosi vya zimamoto kutokana na miundombinu ya
sasa kuwa mibaya ambayo pia inasababisha magari ya zimamoto kutofika katika
maeneo ya matukio kwa wakati.
“Tumekuwa
tukishuhudia mara kadhaa moto unapotokea magari ya zimamoto yanashindwa kufika
kwa wakati na hiyo ni kutokana na miundombinu kuwa mibovu. Ni kwanini serikali
isione umuhimu wa kununua Chopa ili zitumike kuzima moto kuokoa maisha na mali
za watu?,” alihoji.
Akijibu,
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima, alisema
wanakubaliana na ushauri huo na kwamba fedha zitakapopatikana watanunua Chopa
hizo na kuziweka katika miji mikubwa.
Awali
katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalum, Fakharia Shomari Khamis (CCM),
alisema wananchi wengi hawajui kuwa Kikosi cha Zimamoto ndicho chenye wajibu wa
kuzima moto na badala ya yake hukimbilia polisi hivyo kukosa msaada wa haraka
kuzima moto.
Aliitaka
serikali kutoa elimu kwa wananchi ili matukio ya moto yanapotokea watoe taarifa
haraka kwenye vikosi hivyo.
Akijibu,
Silima alisema Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji ndicho chenye wajibu na dhamana
ya kupewa taarifa za ajali na majanga.
Alisema
katika kuhakikisha wananchi wanafahamu juu ya utoaji wa taarifa za ajali na
majanga, kikosi hicho kinaendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia vyombo
mbalimbali vya habari.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment