Mbunge
wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka amemshambulia Mbunge wa Kawe
(Chadema), Halima Mdee pamoja na baadhi ya vyombo vya habari kwamba vinatumiwa
na wabaya wake kumkashifu katika utendaji wake.
Profesa
Tibaijuka alitoa shutuma hizo wakati akihutubia wananchi wa Kata ya Bureza.
Alisema alikumbwa na kashfa ya Escrow, kutokana na kupata fedha kutoka kwa kaka
yake Rugemalila (James) alizompa kusaidia shule anayoisimamia.
Alikanusha
tuhuma zilizotolewa na Mdee bungeni dhidi yake kwamba alipokuwa Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kabla ya kuvuliwa wadhifa huo, alikuwa
mporaji wa mali za wananchi hasa kumiliki ardhi kubwa.
Alidai
kuwa katika kashfa hiyo, kitendo cha kusema fedha aliyoipata ni ya mboga kwa
maana ni ndogo imetafsiriwa na kutumiwa na vyombo vya habari, hasa magazeti
kumchafua zaidi ndani na nje ya Tanzania.
“Nasema
hapa mbele yenu na waandishi wa habari wapo hapa, magazeti yanafanya biashara
kupitia kwangu kwani wanapoandika habari zangu magazeti yananunulika kwa haraka
siku husika,” alisema Profesa Tibaijuka.
Alilitaja
Mwananchi na magazeti mengine pamoja na baadhi yaliyaitwa kuwa ni ya uchwara
ambayo alidai kuwa yamenunuliwa na wabaya wake.
Alidai
kuwa Mdee alidanganya bungeni kuwa Profesa Tibaijuka ni mporaji ardhi za
wananchi kuanzia jimboni na kama isingekuwa ni kinga ya mbunge kutoshtakiwa,
angemfungulia mashtaka mahakamani.
Alisema
waandishi wa habari wa magazeti hawaandiki mambo mema aliyofanya jimboni badala
yake wamesimama kwenye kashfa ya Escrow lakini yeye hafanyi maendeleo yake kwa
fedha hizo, bali ana pensheni ya Umoja wa Mataifa (UN).
“Fedha
nilizopata Umoja wa Mataifa bado ninazo na Halima Mdee tutakuja kukutana mbele
ya safari kama ni pesa ya kula bado ninayo na ile ya Escrow ya Rugemalila ni
kuhemea mboga acheni kudanganyika,” alisema Profesa Tibaijuka.
Aliwaomba
wananchi wa kata hiyo kumuunga mkono kwani licha ya kudaiwa kuwa ana umri
mkubwa hivyo awaachie vijana, bado yumo na atagombea tena kuwaongoza wananchi
akiwa mbunge.
Mdee
ajibu mapigo
Akijibu
shutuma dhidi yake Mdee alisema alichokisema ni cha kweli na kwamba anao
ushahidi kuthibitisha madai yake hayo.
“Asiweweseke
kwa kuwa hilo suala la uporaji wa ardhi ni la kweli na wala sikumuonea.”
0 comments:
Post a Comment