Wakati
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikielekea katika hatua ya kuteua mgombea urais wa
chama hicho, mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru, amefyatuka na
kusema urais ni hatima ya Watanzania hivyo lisifanywe mchezo kuwa mtu yeyote
anaweza kuucheza.
Amesema si vizuri watu waliopewa vyeo ndani ya CCM kuendelea kukitumia chama kwa mambo yao binafsi.
"Kama wana mashaka chama hiki kina historia, vyema wakatutafuta watu ambao tupo, watu tunaojua mambo ya chama," alisema.
Alisema wanaofanya jitihada za kuunda mazingira ya kukitafutia chama kushindwa, wanataka historia ya CCM iishie katika awamu ya nne.
Kingunge ambaye alikuwa miongoni mwa wanachama waliomdhamini Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, katika Wilaya ya Kinondoni, alisema yupo ndani ya chama hicho kwa miaka 60 sasa, ameona mengi ya mkoloni na Tanzania.
"Asilimia kubwa ya Watanzania ni maskini na chama chetu tangu mwanzo tulisema tutapambana na umasikini...Pamoja na mambo mazuri yaliyofanywa lakini sio mwisho, tunahitaji uongozi utakaotutoa katika umaskini na linawezekana hilo," alisema Kingunge.
Alisema ni mwiko kumhukumu mtu kabla ya vikao kwani haijawahi kufanywa hivyo mwaka 1995 na 2005, na hawatafanya hivyo mwaka huu
"Wakifanya hivyo tutakataa, tunataka mchakato ufuate taratibu zilizowekwa, nimemsikia kiongozi wetu mmoja alizungumzia katika Tv kuwa mtu hawezi kwenda kujinadi yeye binafsi bali chama ndio kinamnadi...Mimi nataka niseme kuna ngazi mbili; mwanachama anatakiwa kujinadi ndani ya chama na ndiyo tumefanya hivyo miaka yote kwa mujibu wa taratibu na ndivyo wanavyofanya kina Lowassa, anajinadi kwa wanachama," alisema.
Alisema baada ya mkutano mkuu wa kumpata mgombea, atanadiwa na chama hivyo si vizuri watu waliopewa vyeo kutumia chama kwa mambo yao binafsi.
"Katika utaratibu wetu tuna misingi ya kuamua na mwenyekiti wa chama chetu, Jakaya Kikwete, alitangaza yeye mwenyewe kwamba tutafute mgombea anayekubalika ndani na nje ya chama na ndio msimamo wa chama...CCM inamtafuta mtu anayekubalika ili kuleta ushindi ndani ya chama, wale wanaojitahidi kufanya hivyo kukitafutia chama kushindwa wanataka historia ya Chama Cha Mapinduzi iishie katika awamu ya nne," alitahadharisha.
Alisema suala la urais lisifanyiwe mizengwe, watu waulizwe wanamtaka nani na nani atakayewatatulia changamoto zao.
"Watu wenye busara wanafuatilia mambo yanavyoenda na wameona, wagombea wapo wengi, wenye macho wapo wengi na wanaona, hivyo watu watulize vichwa na kuamua ni nani watamchagua," alisema Kingunge.
Naye Mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa huo, Hemed Mkali, alisema Lowassa ndiyo Rais kwani anakubalika na wananchi wengi hivyo ni vyema viongozi wakaliangalia hilo.
"Kama wakipeleka kiatu cha polisi hawatakichagua hivyo CCM ikipeleka kiongozi ambaye hakubaliki watambue wananchi watamkataa,"alisema Mkali.
LOWASSA: NITAUNDA SERIKALI RAFIKI
Akizungumza baada ya kudhaminiwa na wanaCCM 212,150, jijini Dar es Salaam, Lowassa alisema endapo atateuliwa kuwa rais ataunda serikali ambayo ni rafiki kwa masikini na matajiri.
Alisema yeye ni rafiki wa wanyonge na anachukizwa na vitendo vya wamachinga na mama ntilie kufukuzwa ovyo.
"Siruhusiwi kusema maneno mengi lakini nawashukuru sana kwa kunidhamini hapa Dar es Salaam, udhamini wenu nyie ndio mnaoongoza katika nchi nzima kwa kunipatia wadhamini wengi, heshima mlionipa nitaitunza na kuienzi katika maisha yangu," alisema Lowassa.
"Tunaheshimu kazi zilizofanywa na waliotutangulia sisi tunachukua kijiti tu cha kuboresha nina uwezo na nia ya kubadilisha nchi hii...mwaka 1995 Mwalimu aliwaambia Watanzania wananchi wanayataka mabadiliko wakiyakosa ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM, mimi naamini ndani ya CCM tunaweza kuleta mabadiliko haya na mimi ndio nitakayeyaleta," alisema.
Alisema endapo atafanikiwa katika safari yake ya kusaka urais, moja ya ajenda itakuwa ni kuboresha miundombinu ya jiji hilo ndani ya miezi sita.
Alisema wakati akiwa Waziri Mkuu alijaribu kutafuta ufumbuzi wa suala hilo na kuongeza kuwa miundombinu hiyo itaenda sambamba na ujenzi wa nyumba milioni moja kila mwaka ili Dar es Salaam iwe ya kisasa.
Aidha, alisema akifanikiwa atahakikisha inatungwa sera kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizo ili jiji liwe na hadhi ya kipekee.
Alisema kutakuwapo na Waziri wa Dar es Salaam atakayeshughulikia matatizo ya jiji hilo ambapo akilala akiamka anawashughuliki bila kusubiri maamuzi yakatolewe Dodoma.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Asaa Simba, alisema kudhaminiwa kwa Lowassa na wanachama wengi kunatokana na kukubalika kwa matendo na utendaji wake.
" WanaCCM Ilala wamefurahia sana kitendo cha wewe kutangaza kugombea na wamejitokeza wengi kukudhamini mpaka sasa wamekudhamini 44,799 hapa Ilala," alisema Simba.
Aidha alisema ishara ya wananchi ni kwamba CCM na wananchi wanamtaka Lowassa na tayari viongozi walishasema achaguliwe mtu anayekubalika na kwa sasa yeye ndiyo anayeonekana.
Naye Mbunge wa jimbo la Ilala, Mussa Zungu alisema Lowassa ndio mwarobaini wa matatizo ya wamachinga, mama ntilie na Bodaboda.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam alhaji Ramadhani Madabida, alisema ameonesha dhamira ya kutaka kuwatumikia Watanzania na moja ya sifa za kiongozi ni kuwa mstahimilivu na kuhilimili mikikimikiki.
Aidha alimfananisha Lowassa na Mtume Muhammad kwamba ni kiongozi mvumilivu.
Alipowasili Dar es Salaam, baadhi ya barabara zilifungwa ikiwamo barabara ya Nyerere kutokana na msafara mkubwa.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment