Mbunge
wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohammed (pichani), anatarajia kukabidhiwa
rasmi kadi ya uanachama wa Chama cha Alliance for Democratic Change
(ADC), Julai 15, mwaka huu Visiwani Zanzibar, siku ambayo pia atatangaza
rasmi kuwania urais kupitia chama hicho.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama hicho Said
Miraaj, alisema baada ya kukabidhiwa kadi na kutangaza nia ataanza ziara yake
ya kujitambulisha kwa wananchi.
Alisema
mpaka sasa watia nia waliojitokeza kuomba kuteuliwa kupeperusha bendera ya
chama hicho kwa upande wa Zanzibar ni Hamad Rashid pekee.
Miraaj
alisema bado milango haijafungwa na kuwaomba watu wengine wanaohitaji kuwania
nafasi hiyo kwa upande wa Zanzibar wajitokeze kwa kuwa mwisho wa siku
chama ndicho chenye maamuzi ya mwisho ya nani agombee na nani asigombee
kulingana na sifa zao.
Kwa upande
wa Tanzania Bara, Miraaj alisema tayari wameshajitokeza wagombea watatu wa
nafasi ya urais ambao nao wanataraji kutangaza rasmi nia yao hiyo mwezi ujao.
Aliwataja
watangaza nia hao kuwa ni Abubakari Lakeshi, Emmanuel Faustine na
Lutalosa Yemba (maalufu kwa jina la Chifu Yemba) ambao nao baada ya
kutangaza wanatarajia kuzunguka mikoa mbalimbali kujitambulisha kwa wananchi
mwezi ujao.
Pia
alisema pamoja na kujitokeza kwa watia nia hao, lakini bado wanapokea watia nia
wengine watakaojitokeza kuwania nafasi hiyo ndani ya ADC.
Miraaj
alisema Chama kimeweka utaratibu wa kuwasaidia watia nia wa nafasi ya
urais katika kulipia gharama zote zitakazotumika wakati wanatangaza nia ili
kuepusha kuonyeshana ubabe kati ya watia nia hao walio nacho na wasio nacho.
Kwa upande
wa nafasi ya Ubunge, Miraaj alisema chama kimepanga kusimamisha wabunge zaidi
ya 100 na kwamba mpaka sasa watu waliojitojeza kuwania nafasi hiyo katika
majimbo mbalimbali nchini ni zaidi ya 80.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment