Rais
Jakaya Kikwete ameomba radhi kwa Watanzania aliowakosea wakati wa utumishi wake
wa miaka kumi Ikulu huku akisisitiza hakuna binadamu aliyemkamilifu.
Aliyasema
hayo mwishoni mwa wiki iliyopita, wakati akizungumza kwenye sherehe ya
kuadhimisha miaka miwili ya Upapa wa Baba Mtakatifu Francis iliyofanyika
nyumbani kwa Balozi wa Vatican nchini, Oysterbay jijini Dar es Salaam na
kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali.
Rais
Kikwete alitumia pia nafasi hiyo kuwaaga viongozi hao wakuu wa Kanisa Katoliki
akiwasisitizia kuwa anaacha nyuma nchi yenye amani na utulivu huku
akiwataka viongozi hao kufanyakazi vizuri na kiongozi mpya na kudumisha amani
na utulivu wa kijamii kama walivyofanya kwake.
Alisema
anaamini kuwa hakuna asiyekosea katika maisha kwani yeye alijaribu alivyoweza
na kwa kadri ya uwezo wake lakini inawezekana kukawa na watu ambao aliwakosea
hivyo wamsamehe na waelewe ukomo wa uwezo wa binadamu.
“Napenda
pia kusisitiza kuwa hakuna binadamu aliyekamilifu na kwa wale ambao niliwakosea
naomba waelewe ukomo wa uwezo wa binadamu naacha nyuma nchi yenye amani
na utulivu, nchi ambayo inapitia katika kipindi cha ustawi wa kiuchumi na
kijamii ambao haujapata kutokea katika historia ya Tanzania," alisema na
kuongeza kuwa:
"Nina
hakika kuwa mrithi wangu ataendeleza kazi nzuri ambayo nimeifanya katika miaka
10 iliyopita hasa ile ya kujenga na kuimarisha uhusiano kati ya Dola na
Kanisa.”
Aidha,
aliwaomba viongozi wa dini nchini kusaidia kuendeleza jadi nzuri ya Tanzania
kwa kuhakikisha nchi inabaki na amani, kabla, wakati na baada ya
Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu, 2015. Alilishukuru
Kanisa Katoliki nchini kwa kuendeleza ushirikiano wake na serikali wa kutoa
huduma za jamii katika maendeleo mbali mbali likiwamo la elimu na afya.
Kikwete
pia alisema kuwa kwa sababu Dola na Kanisa ni taasisi zinazoendeshwa na
binadamu, inatokea wakati mwingine uhusiano kati ya taasisi hizo mbili ukapitia
katika mawimbi lakini ni uhusiano unaoendelea kuwapo na kuimarishwa.
Wengine
waliohudhuria sherehe hiyo iliyoandaliwa na Balozi Askofu Mkuu Francisco
Padalli, ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Katoliki Dar es Salaam,
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na maskofu wa karibu majimbo yote ya
kanisa hilo nchini.
“Kila
miaka mitano, Tanzania hupiga kura kupata ridhaa ya wananchi ya kuongoza.
Makabidhiano ya madaraka katika Tanzania limekuwa suala la amani na tunabakia
mfano wenye kung’ara katika Afrika kwa kuruhusu makabidhiano ya amani," alisema.
"Kwa
utaratibu huu mzuri, nitamaliza muda wangu wa uongozi na kukabidhi madaraka kwa
rais mpya. Naamini kuwa Kanisa Katoliki litasaidia sana kuhakikisha mchakato
wetu wa uchaguzi na makabidhiano ya uongozi vinakuwa vya amani.”
Kuhusu
miaka miwili ya uongozi wa Papa Francis, Kikwete, alisema kiongozi huyo
ameleta matumaini mapya duniani, ujumbe mpya wa amani, heshima kwa utawala wa
sheria amani na utulivu.
“Ujumbe
wake kuhusu changamoto nyingi duniani, likiwamo lile la tabianchi, umeongeza sauti
yenye nguvu sana kwa namna dunia yetu inavyoendeshwa.”
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment