Zitto: Uuzaji benki ya NBC ulifanywa ovyo ovyo.

02:53 by Kwetuhouse Media


Chama cha ACT-Wazalendo kimesema ili nchi iweze kujitegemea kiuchumi ni lazima benki kubwa zimilikiwe na Watanzania tofauti na ilivyo hivi sasa kwa benki hizo kumilikiwa na wageni huku ikitaka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) irejeshwe kwa Watanzania. 

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki wilayani Muheza mkoani Tanga na Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe katika mkutano wa hadhara.

Alisema utaifishaji wa mabenki uliofanyika mwaka 1967 na kuundwa kwa NBC, Benki ya Nyumba na Benki ya Maendeleo Vijijini ilikuwa ni maamuzi ya msingi kwa maendeleo ya nchi.

Alisema ubinafsishaji wa NBC na kuuawa kwa Benki ya Nyumba ilikuwa ni maamuzi yasiyo na msingi hali ambayo haijawahi kutokea katika nchi baada ya kupatikana uhuru.

Alibainisha kuwa malengo ya kujenga uchumi shirikishi wenye uhuru mkubwa katika soko la mitaji hayawezi kufikiwa bila ya kuwa na benki zinazomilikiwa na Watanzania wenyewe. 

Alisema Chama cha ACT-Wazalendo kitahimiza. NBC kurejeshwa kwenye mikono ya Watanzania kwa kumilikiwa na serikali kwa asilimia 50, wananchi na taasisi za wananchi kupitia soko la mitaji nusu iliyobakia.

"Ubinafsishaji wa NBC ulifanywa holela na benki iliuzwa kwa bei ya kutupwa kimsingi, msimamo huu wa ACT -Wazalendo unaungwa mkono na kazi iliyofanywa na kamati ya Bunge ya PAC iliyoagiza ukaguzi maalumu kwenye mchakato wa ubinafsishaji wa Benki hiyo na hata Mwalimu Nyerere alikufa na kinyongo cha Benki hii," alisema Kabwe. 

Alisema wakati NBC ikiwa inaendelea na shughuli zake kulitokea hasara ya dola za Kimarekani milioni 143 zilizotokana na mikopo iliyotolewa kwenye sekta ya usafirishaji.

Alisema mikopo hiyo ilikuwa ya kitapeli na serikali ilifidia hasara hiyo kwa kulipa nyongeza ya mtaji katika benki sawa na kulipia hasara ambayo waendeshaji wa benki hiyo waliifanya.
CHANZO: THE GUARDIAN

0 comments:

Post a Comment