WATANZANIA TAKRIBANI MILIONI 24 WATAPIGA KURA 2015.

16:27 by Kwetuhouse Media


 OFISI ya Taifa ya Takwimu imetoa makadirio ya idadi ya watu wanaotarajiwa kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015 ambao wanakisiwa kuwa watafikia milioni 24.2 nchi nzima.

Taarifa hizo ni makadirio ya idadi ya watu wanaostahili kupiga kura katika majimbo ya uchaguzi Tanzania kwa mwaka 2015. Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, idadi ya wapigakura waliojiandikisha ilikuwa 20,137,303, lakini waliopiga kura Oktoba 31 mwaka huo walikuwa 8,626,283 sawa na asilimia 42.84 ya wapiga kura wote waliojiandikisha.

Takwimu hizi zimetolewa katika ngazi ya Mkoa, Wilaya, Jimbo la Uchaguzi na Kata au Shehia kama yalivyokuwa mwaka 2010. Makadirio ya idadi ya wapigakura yametokana na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012.

Kwa mujibu wa ripoti iliyo kwenye kitabu maalumu cha takwimu za wapiga kura mwaka huu, ambayo nakala yake imepatikana kupitia Ofisi ya Takwimu ya Mkoa wa Arusha, idadi hiyo imepatikana kwa kutumia mbinu za kidemografia zinazohusisha mabadiliko katika viwango vya uzazi, vifo, uhamaji na uhamiaji katika ngazi ya Taifa, Mkoa, Wilaya, Majimbo ya Uchaguzi na Kata au Shehia husika.

Inakadiriwa kuwa ifikapo siku ya uchaguzi, Tanzania itakuwa na watu wapatao 48,522,229 ambapo watakaokuwa na umri wa kupiga kura watakuwa ni watu 24,252,927 iwapo wote watafanikiwa kuandikishwa upya.

Mkoa wa Dar es Salaam wenye majimbo nane unatarajiwa kuwa na wapiga kura wengi zaidi watakaofikia milioni 3, ukifuatiwa na Mbeya itakayokuwa na wapiga kura milioni 1.5, Mwanza milioni 1.4 na Morogoro itakayokuwa na wapigakura milioni 1.3 katika nafasi ya nne.

Mikoa mingine inayotarajiwa kuwa na wapiga kura wengi ni pamoja na Kagera itakayokuwa na wapigakura milioni 1.2, Tabora inayokadiriwa kuwa na idadi ya wapiga kura milioni 1.1, Tanga nayo kwa idadi kama hiyo ya milioni 1.1 pamoja na Dodoma itakayokuwa na wastani wa wapigakura milioni moja.

Mkoa wa Kilimanjaro unatarajiwa kuwa na wapiga kura 976,000 katika nafasi ya tisa na hatimaye Arusha kufunga kumi- bora ikiwa na matarajio ya wapiga kura wapatao 944,000. Idadi ya wapigakura watarajiwa kwa mikoa mingine ni kama ifuatavyo:
Mara (834,000), Geita (808,000), Ruvuma (783,000), Mtwara (773,000), Shinyanga (762,000), Manyara (741,000), Simiyu (714,000), Singida, (698,000), Pwani (644,000), Iringa (524,000), Rukwa (472,000) na Njombe (393,000).

Mkoa mpya wa Katavi, ambao una idadi ya wakazi wapatao 609,000 ndio utakuwa na idadi ndogo zaidi ya wapigakura kwa Tanzania bara wakitarajiwa kuwa 271,000. Huko visiwani mkoa wa Mjini Magharibi unatarajiwa kuwa na wapigakura 347,000, Kaskazini Unguja 104,000, Kaskazini Pemba 103,000, Kusini Pemba 95,000 na Kusini Unguja 69,000.

Maandalizi ya kitabu cha idadi tarajiwa ya wapigakura yameshirikisha maofisa kutoka Wizara, Idara na Taasisi za Serikali ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar, pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Tume ya Uchaguzi Zanzibar na Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC).

0 comments:

Post a Comment