MILIO ya risasi
ilisikika katika vituo vya uandikishaji kura katika kata ya Sokoni One jijini
hapa, baada ya kuibuka kwa vurugu zilizohusisha vijana wa Chadema na wenzao wa
CCM, chanzo kikitajwa madai ya kuwepo kwa watu ambao sio wakazi wa eneo hilo
kutaka kujiandikisha.
Vurugu hizo
zilisababisha takribani watu 15 kukamatwa akiwemo Mbunge wa Jimbo la Arusha
Mjini, Godbless Lema (Chadema) ambaye hata hivyo baadaye aliachiwa huru.
Alishikiliwa kuanzia saa 1:30 usiku hadi saa 4:00 usiku juzi.
Patashika hiyo
ilichukua zaidi ya saa moja, kwani baadhi ya polisi waliokuwa na silaha za moto
aina ya bastola walifyatua risasi hewani kwa lengo la kutawanya vurugu hizo,
lakini hali ilikuwa mbaya zaidi hadi polisi walipoongezwa na kufanikiwa
kutuliza ghasia hizo.
Wakati hayo yanatokea
Lema alisisitiza kuwa kamwe hawezi kukubali kutohamasisha wananchi kwenda
kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura licha ya kudai kuwa, kundi
la vijana wanaosadikiwa kuwa wa CCM wamempiga mawe sambamba na watu wengine
waliojitokeza kujiandikisha katika kata mbalimbali.
Hata hivyo, upande wa
vijana wa CCM, umedai wenzao wa Chadema ndio chanzo cha vurugu, kwani
wameonekana wakisambaza makundi ya vijana wasiostahili kuandikisha katika vituo
mbalimbali.
Lema ajitetea Akizungumzia
kukamatwa kwake na polisi wa kata ya Osunyai kutokana na vurugu zilioibuka,
alidai alikuwa akitoa taarifa za uongezwaji wa mashine za BVR kwa wananchi na
kuwapa moyo kuwa watulivu wakati wa uandikishwaji sambamba na kutunza
vitambulisho hivyo kwa ajili ya kupiga kura mwaka huu katika uchaguzi mkuu wa
rais, wabunge na madiwani.
Alisema wakati
akiendelea kuwapa moyo wananchi na kusema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
imeongeza mashine za BVR, ghafla aliona vijana anaodai wamekodishwa kufanya
vurugu kwenye vituo mbalimbali vya kujindikisha na ndipo alitoa taarifa Polisi,
lakini badala ya kukamata vijana hao alikamatwa yeye na vijana wengine na
kuweka mahabusu.
NEC iliruhusu
uandikishaji kuendelea hadi saa mbili usiku kutokana na wingi wa watu wanaostahili
kuandikishwa. Hata hivyo mmoja wa wafuasi wa CCM aliyejitambulisha kwa jina la
Abdi Marijani maarufu kwa jina la ‘`Mutu’ alisema Chadema wamekuwa wakileta
watu ambao sio wakazi Jiji la Arusha kutaka kujiandikisha hali iliyopingwa na
vijana hao.
Mutu alisema CCM
ilikuwa imepewa taarifa juu ya njama za Chadema za uchomekeaji watu katika kila
kata na chama kikaweka vijana imara katika kila kituo wakiwa na mabalozi ambao
ndio wenye jukumu la kujua mkazi wa eneo husika.
Akizungumza na
waandishi wa habari mjini hapa jana, Lema alisema juzi akiwa kata ya Osunyai
alishangaa kuona kundi la vijana wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser
lenye namba za usajili T 122 ATR ambalo alidai wakati mwingine gari hilo
lilibadilishwa namba na kusomeka T 122 ABR wakishuka ghafla na kuanza kumpiga
mawe na kuwapiga vijana wengine 25 ambao walikuwa katika kituo hicho.
Alisema wakati tukio
hilo likitokea alitoa taarifa kwa Mkuu wa Upelelezi wa wilaya OC/CID, Faustine
Mwafele ili kuwaelezea tukio hilo, lakini polisi walifika eneo la tukio badala
ya kuwakamata vijana hao walimkamata yeye na vijana waliokuwepo kisha kuwaweka
chini ya ulinzi.
Alisema inaonekana
kundi hilo linaonekana lipo juu ya sheria watu wanafanya fujo za waziwazi, huku
mbunge akigeuziwa `na kusulubiwa.
Alisema kwa kuwa yeye
ni mbunge, hawezi kuacha kuhamasisha wananchi wake kujiandikisha badala yake
chama chao na viongozi wa chama wataendelea kuhamasisha watu kujitokeza
kujiandikisha sambamba na kuhamasisha watu wasikate tamaa katika kujiandikisha
kwa sababu ni wajibu wao wa kisheria, kisiasa na kidemokrasia.
Aliongeza kuwa
udhalilishwaji sasa umefika mwisho, hivyo alitoa rai kwa vijana wa chama hicho
kuchukua hatua ya kuwalinda viongozi wao, kulinda demokrasia na mali zao.
Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Arusha, Liberatus Sabas hakupatikana kuzungumzia tukio hilo, licha ya
kutafutwa kupitia simu yake ya mkono ikiwa ni pamoja na kutumiwa ujumbe mfupi
wa maandishi.
Wasemavyo CCM
Akizungumzia hilo, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Arusha, Feruz Banno alisema
vurugu zilianzishwa na vijana wa Chadema kwa kuwapiga vijana wa CCM na kupiga
risasi hewani hovyo bila ya sababu za msingi.
Banno alisema dola
Arusha inapaswa kuwa makini, kwani hali inaweza kuwa mbaya zaidi iwapo hilo
halitadhibitiwa na kuwafanya watu wengine kushindwa kwenda kujiandikisha kwa
kuogopa vurugu.
Alisema kutokana na
vurugu zinazofanywa kwenye baadhi ya vituo vya kujiandisha na baadhi ya
viongozi wa Chadema ili kudhibiti wazee na akinamama wanaokwenda kujiandikisha
kwenye vituo hivyo.
Alisema kwa sasa uandikishaji
unafanyika katika kata za Terati, Murieti, Olusunyai, Moshono, Sinoni na Sokoni
One, lakini baadhi ya vijana wa chama hicho wamekuwa wakisafirishwa kwa magari
kutoka kata tofauti na hizo na kupelekwa eneo hilo kwa ajili ya kujiandikisha .
Ulinzi Kwa upande wake
Marijani, alisema kutokana na udhibiti uliowekwa na makamanda wa CCM vituo vya
kupigia kura wamebaini kuwa viongozi wa Chadema na vijana wao wamekuwa wakileta
vurugu katika kila kituo ili zoezi hilo lisiweze kufanikiwa.
“Tumeweka ulinzi kila kituo
na hiyo itakuwa ikifanyika katika kata zote za Jiji la Arusha kwani hiyo
itasaidia kupata wakazi halisi wa eneo husika na sio mamluki,” alisema Mutu.
0 comments:
Post a Comment