Chama Cha
Mapinduzi (CCM), kimeungana na wadau wa habari kwa kuitaka serikali kukubali
kuondoa Muswada wa Habari wa mwaka 2015 bungeni ili kuurudisha kwa wadau ili
uweze kujadiliwa upya.
Katibu wa
Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye (pichani), alitoa kauli hiyo juzi wakati
akiwahutubiwa wananchi wa jimbo la Misungwi, mkoani Mwanza, ikiwa ni sehemu ya
ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, katika mikoa ya kanda ya ziwa.
Nape
alisema si vyema serikali kulazimisha muswada huo kujadiliwa bungeni kabla ya
wadau wa habari hawajaridhika nao, kwani lengo ni kusaidia serikali na wadau wa
habari na si vinginevyo.
Alisema
kumekuwa na mjadala mrefu kuhusu muswada huo wa habari, hali ambayo
imesababisha kuwa na msuguano mkubwa kati ya Serikali na wadau wa habari nchini
na hiyo ni kutokana na vifungu vilivyopo ndani yake ambavyo vinaikosesha
haki ya kupata habari tasnia hiyo.
Nape
alisema kutokana na hali hiyo, kuna haja ya serikali kuwasikiliza wadau wa
habari kwa sababu kama sheria zinatungwa na serikali huku wadau wakizilalamikia
litakuwa siyo jambo jema.
“Kuna
vipengele ambavyo si sawa kwa mfano, mwanahabari anataka taarifa kutoka
serikali atume maombi ndani ya mwezi ndipo yajibiwe na pia mtoa majibu ana
hiari hiyo habari itoke au isitolewe, sasa ina maana gani kwa jamii na tasnia
kwa ujumla kama taarifa itatoka ndani ya mwezi hakuna habari hapo,” alisema
Nape.
Aliongeza
kuwa kama ikitokea wadau wameikataa sheria hiyo, lakini serikali ikalazimisha
ni wazi kuwa sheria hiyo utekelezaji wake utakuwa mgumu.
Mambo
yanayolalamikiwa na wadau katika muswada ni pamoja na vifungo ambavyo vinambana
mwandishi kutoa habari hadi pale aliyetoa habari atakapomtaka kufanya hivyo.
Pia sheria
hiyo inamtaka mwandishi wa habari akienda kuchukua habari katika ofisi ya
Serikali apeleke maombi ndani ya siku 30 na hata akifanikiwa kupata
habari hiyo, hawezi kuitoa hadi aruhusiwe na kama ataitoa bila kibali anaweza
kufungwa kifungo cha miaka mitano jela.
Muswada
wa Sheria ya Kupata Habari wa Mwaka 2015 unatarajia kuwasilishwa katika Bunge
la Bajeti linaloendelea mjini Dodoma.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment