Rasimu iliyopitishwa na
Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma, ni kielelezo cha wazi cha ukweli huu
kwamba ujinga ni mtaji mkubwa wa kisiasa unaotumiwa na chama tawala kwa
wananchi wasiojitambua.
Hawa ni wananchi
wanaoshabikia kibubusa kila kitu kinachopendekezwa na uongozi wa CCM, hata kama
ni kwa masilahi binafsi ya viongozi wachache.
Wataalamu wa elimu
wanasema kwamba ‘maarifa ni nguvu’ Mtu ukiwa na elimu na maarifa ya kujitambua
na kutambua haki zako na nini inaendelea katika maisha yako, mazingira na nchi
yako basi wewe umekombolewa.
Hata hivyo, kuendelea
kuishi katika lindi la ujinga na giza la kutojitambua, ni mtaji wa
kudanganganywa na kutawaliwa.
Bunge la Katiba mpya
liliendeshwa kwa msingi ya udanganyifu, ubabe na kuukwepa ukweli uliopendekezwa
na wananchi katika Tume ya Warioba. Daima tunasema kwamba uongo hauwezi kuzaa
ukweli hata siku moja.
Ona pia suala la
watangazania wa CCM, wote wanaongea lugha nzuri na kuonyesha kutetea masilahi
ya wananchi, lakini walikuwa wapi na wamefanya nini katika kipindi chote hicho?
Wananchi waliojitambua
wanauliza, kwa jinsi nchi ilipofikia chini ya chama tawala, kuna haja gani ya
kuendelea kuichagua tena CCM inayoonyesha wazi kushindwa kuongoza nchi?
Watanzania wameahidiwa
usawa wa 50/50 na katiba mpya. Hili linawezekana katika nchi kama ya Tanzania,
wakati Ulaya na Marekani kwenyewe bado wanawake wanalalamika? Kuipitisha katiba
hii ni sawa na “kuchukua kisu na kijichinja sisi wenyewe, au kuchukua bunduki
na kujipiga risasi mguuni.
Tunahitaji katiba
itakayoleta mabadliko katika nchi yetu na katiba hii pendekezwa, haina uwezo wa
kubadilisha lolote. Hili ni suala la mfumo. Kila atakayekuja kuwa Rais kutoka
CCM lazima alinde na kuendeleza mfumo huu wa unaowalinda wachache.
Katiba ya CCM
Rasimu ya CCM
iliyopitishwa Bunge la Katiba kwa ujasiri mkubwa imeondoa uwazi na uwajibikaji
kwa viongozi wake. Katiba pendekezwa inataka kuendeleza usiri na viongozi
kujifanyia mambo kiholela holela kama wanavyotaka wao kwa manufaa yao, familia
zao na marafiki zao.
Katiba hii ikipita
wananchi hamtakuwa na uwezo wa kuwawajibisha viongozi wenu kama
yalivyopendekeza maoni ya Rasimu ya Mzee Warioba.
CCM inakataa elimu
kubwa kwa wabunge na badala yake inasema mtu akijua kusoma na kuandika basi
inatosha, Hili ni balaa. Je, huku siyo kutumia mtaji wa ujinga ili kuwatawala
wananchi?
Kinachoonekana katika
nchi yetu ni kwamba Watanzania wanatawaliwa na watu wasio na elimu ya kutosha,
mbunge wa darasa la saba anakwenda kumtungia sheria wakati nchi ina wasomi
kibao wanazurura tu mitaani.
Je, mbunge mbumbumbu
atasomaje mikataba na kuweza kuichanganua? Pia, mikataba yenyewe ni ya siri,
maana yake ni kuendeleza ufisadi mkubwa wa rasilimali ya wananchi.
Mjue kwamba kupitisha
katiba hii kuna madhara makubwa kwa uchumi wa Tanzania; ndiyo kusema pamoja na
kuwa na rasilimali za gesi, madini, mbuga za wanyama pori umaskini utaendelea
kuwaandama wananchi na Taifa kwa jumla.
Katiba inaendelea
kuwadanganya wanawake eti watamiliki ardhi, uwezo huo wataupata wapi? Pia ardhi
ya kumiliki ipo wapi jamani kwa maana ardhi kubwa wameshapewa wawekezaji wa
kutoka nchi za nje
Aidha, wanaomiliki
ardhi hiyo wengi ni viongozi na vigogo wa Serikali, je, wanawake mtamiliki nini
sasa? Hizi ni siasa za kutaka kupata kura kutoka kwa watu masikini na
wasiojitambua.
Kwa vile wanawake ndiyo
mtaji mkubwa wa kura za CCM, basi wanajaribu kuwachota kwa kuwadanganya kuhusu
ardhi kama walivyowachota Waislamu na suala la mahakama ya kadhi ambalo ni
ndoto kuingia katika katiba, kwa sababu kila dhehebu lipo macho na suala la
dini moja kupewa mamlaka ya kikatiba.
Kiukweli rasimu hii
imeweka mzigo mkubwa wa baraza la mawaziri tofauti na rasimu ya Warioba ambayo
ina maoni ya wananchi wenyewe.
Pia rasimu hii imependekeza
Rais na makamu wa rais watatu, je, kule kukataa serikali tatu kwamba ni gharama
kumbe hawakuwa na hoja kabisa. Wananchi tafakarini jinsi mtakavyokamuliwa fedha
kuiwezesha Serikali hii kubwa badala ya kupunguza gharama.
Katiba hii itakuwa
mbaya kuliko ya sasa ndiyo kwa maana Maaskofu wa Jukwaa la Wakristo wameikataa
kama shetani na mambo yake.
Sasa ni wazi kwamba
Serikali ya CCM haina nia thabiti ya kumkomboa mwananchi masikini kiuchumi,
kisiasa, kiutamaduni wala kifikra. Serikali haina utashi huo inachotaka ni
kuendeleza ulevi wa madaraka.
Ni kwa sababu hii hata
watiania wa kiti cha urais kupitia CCM wote wameogopa kuongelea suala la Katiba
Inayopendekezwa pamoja na Mahakama ya Kadhi.
Watanzania tutafakari,
tufikiri na tuchukue hatua kwani nchi inaendelea kuliwa na wahenga husema
“wajinga ndiyo waliwao.” Katiba Inayopendekezwa imejaa ubabe, fitina, vitisho,
utumwa, umasikini,ubaguzi, mgawanyika katika jamii na ahadi hewa haina uwezo wa
kuleta mabadiliko yanayokusudiwa na Watanzania wa leo.
Kinachotakiwa ni kwa
umoja wetu bila kujali dini, itikadi wala kabila kusema kwa pamoja katiba
inayopendekezwa “Hapana” katika kura ya maoni siku zijazo.
Ndiyo maana
nawakumbusha Watanzania wenzangu kwamba Katiba Inayopendekezwa haiwezi kuleta
mabadiliko yeyote yale katika nchi yetu pamoja na ahadi nyingi za watangazania
wa CCM. Mungu utusaidie!
0 comments:
Post a Comment