Kikao
cha Bunge kimeahirishwa hadi leo ili kutoa fursa kwa wabunge kuomboleza kifo
cha mwenzao aliyekuwa Mbunge wa Geita (CCM), Donald Max, kilichotokea juzi
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MHN) Dar es Salaam alikolazwa kwa matibabu
baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Spika
wa Bunge, Anne Makinda, alisema taarifa za awali zinaeleza kuwa mwili wa Max
unatarajiwa kuzikwa Jumamosi, Dar es Salaam.
“Waheshimiwa
wabunge nasikitika kuwatangazia kwamba ndugu yetu, Donald Kelvin Max,
ametangulia mbele ya haki, alikuwa amelazwa kwa muda mrefu, lakini jana (juzi)
mchana alituacha...utaratibu wa wale watakaotakiwa kwenda kuzika Katibu wa
Bunge anafanya utaratibu, kwa mujibu wa kanuni zetu siku mwenzetu akifariki
hakutakuwa na bunge,” alisema Makinda. Mbunge wa Busanda ( CCM), Lolesia
Bukwimba, alimuelezea Max kuwa wakati wa uhai wake alikuwa ni mwenye
bidii na alifanya mambo makubwa kwa Mkoa wa Geita ambako alijenga uzio
katika Hospitali ya Wilaya ya Geita, Shule ya Sekondari ya Geita mjini, na
kwamba wananchi walikuwa wakimuamini katika jitihada zake hizo.
“Alijitoa
kwa fedha zake, alisadia wagonjwa katika hospitali ya Geita, wananchi
wananzungumzia na kumkumbuka kwa kipindi chote tangu mwaka 2013 aanze kuugua.
Wanakumbuka fadhila na kazi ambazo amezifanya katika wilaya ya Geita na kazi
nyingi alifanya kabla hajawa mbunge,” alisema.
Mbunge wa
Viti Maalum (CCM), Fatuma Mikidadi, alisema Max alikuwa rafiki wa vyama
vyote, hodari, mwaminifu na mchapakazi.
Alisema
mambo aliyoyasimamia ni watoto, uzazi wa mpango, uzazi salama ambayo,
yaliingizwa katika bajeti, hivyo kuyasaidia makundi hayo.
Naibu
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Steven Kebwe, alimueleza kuwa alikuwa
mchangiaji mzuri na imara katika kujenga hoja na kuzisimamia.
Kebwe
alisema ni masikitiko makubwa kwa kipindi kifupi kupoteza wabunge watatu wa
bunge hilo.
“Ni pigo
kwa nchi yetu hususani Bunge kwa muda mfupi kupoteza watu muhimu watatu, ikiwa
ni katika hatua za mwisho tukielekea kwenye uchaguzi mkuu na ni simanzi
kubwa,” alisema.
Mbunge wa
Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa, alisema Max alikuwa ni mtu mwenye kutoa
ushirikiano na kwamba maradhi yalimfanya kukaa nje ya nchi kwa muda mrefu hadi
aliporudishwa nchini.
“Tumepoteza
mtu ambaye alikuwa mpole, mwenye ushirikino, alipenda maendeleo ya wananchi
wake, mara kadhaa alitoa hoja za wananchi wake, keleke zake zimesaidia mambo
mbalimbali katika jimbo hilo,” alisema.
Tangu
Januari, mwaka huu, wabunge watatu wa CCM wamefariki dunia. Wengine ni
aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba na wa Ukonga, Eugine
Mwaiposa.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment