Mganga
Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa jamiii, Dk. Magreth Mhando akisoma
hotuba ya uzinduzi wa maabara itembeayo kwa ajili ya mafunzo ya
upasuaji. Kulia ni Naibu Balozi wa Ireland nchini, Maire Matthews na
kushoto ni Mkurugenzi wa ECSA anayeshughulikia Afya ya jamii Prof Yoswa
Dambisya.
Mganga
Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa jamiii, Dk. Magreth Mhando akikata
utepe kuzindua maabara ya upasuaji ya mafunzo inayotembea iliyotolewa
kwa chuo kitembeacho cha COSECSA na serikali ya Ireland.
Mmoja
wa walimu ambaye ni daktari bingwa wa upasuaji akitoa maelezo kwa mgeni
rasmi Mganga Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa jamiii, Dk. Magreth
Mhando aliyemwakilisha Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii na Naibu Balozi
wa Ireland nchini, Maire Matthews.
Na Mwandishi wetu
Mganga
Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Magreth Mhando mwishoni
mwa juma alizindua maabara ya upasuaji ya mafunzo inayotembea
iliyotolewa kwa chuo kitembeacho cha COSECSA na serikali ya Ireland.
Alifanyakazi hivyo kwa niaba ya Waziri wa Afya na Ustawi wa jamii, Dk Seif Rashid.
Maabara
hiyo ambayo ni mradi wa majaribio wa chuo hicho wenye lengo la
kufundisha wapasuaji pale walipo imegharimu dola za Marekani 100,000.
Kwa mujibu wa taarifa za COSECSA maabara hiyo itakuwa nchini kwa miezi kama mitatu kabla ya kwenda Kenya na baadae Malawi.
Mradi
huo wenye lengo la kufundisha wapasuaji zaidi kwa kufika eneo ambalo
wanafanyia kazi, ni moja ya miradi ya chuo kitembeacho ambacho toka
kimeanzishwa mwaka 1990 kimeshatoa wapasuaji 200.
Hafla
ya uzinduzi wa maabara hiyo yenye vifaa vya kisasa vya kufundishia na
kufanyia upasuaji ikiwamo ya upasuaji kwa kutumia darubini ulifanyika
katika hospitali ya kumbukumbu ya Hubert Kairuki.
Rais wa COSECSA , Profesa Stephen Ogendo akisoma taarifa kwa mgeni rasmi kabla ya uzinduzi.
Akizindua
maabara hiyo Dk. Mhando alisema kwamba ni matumaini yake italeta
mabadiliko makubwa katika kuwezesha taifa kuwa na wataalamu wengi wa
upasuaji.
Aidha
alisema changamoto ya kutosajiliwa kama chuo kamili wakati mataifa
mengine yamefanya atayafuatilia ili kuweza kuona ya kukiwezesha chuo
hicho kutambuliwa rasmi nchini Tanzania.
Maabara
hiyo mali ya College of Surgeons of East Central and Southern Africa
(COSECSA) iliwasili mapema mwezi huu na jana ndio ilikuwa uzinduzi
rasmi ambao ulishuhudiwa na wanafunzi wa upasuaji, wataalamu na maofisa
mbalimbali wa afya wakiwemo watu wa Mfuko wa taifa wa Bima ya Afya
(NHIF).
Kaimu
mkurugenzi wa Mfuko huo Michael Mhando alisema kwamba wamefurahishwa na
juhudi za wadau wao katika kuimarisha vifaa tiba na utoaji wa
wataalamu.
Alisema anaamini kwamba maabara hiyo ni moja ya mambo muhimu yanayotakiwa kufanywa na wadau ili kuimarisha tiba nchini.
Alisema
kwamba wataangalia namna ya kufanya ili kusaidia huduma hiyo kwani
inahitajika sana vijijini ambako wengi wa watu hawapati fursa ya
kufanyiwa upasuaji hata ule mdogo.
Baadhi ya wadau wa sekta ya afya na wanafunzi waliohudhuria hafla hiyo.
Maabara hiyo yenye uzito wa tani 30 inatarajia kufanya mafunzo ya upasuaji katika hospitali zenye uhusiano na COSECSA.
Aidha maabara hiyo inaweza kufunza wapasuaji 10 kwa mkupuo mmoja.
Kuletwa
kwa maabara hiyo kutoka Ireland ambako kuna uzoefu wa miaka mingi wa
kutumia maabara zitembeazo za upasuaji kumefanikishwa na mahusiano
yaliyopo kati ya Royal College of Surgeons in Ireland (RCSI), Shirika la
misaada la Ireland (Irish Aid) na College of Surgeons of East, Central
and Southern Africa (COSECSA).
Maabara
ya mafunzo ya upasuaji itembeayo ilianzishwa na RCSI kwa mara ya kwanza
duniani mwaka 2006 na kwa uzinduzi uliofanyika dare s Salaam jana
umedhihirisha dhamira njema ya COSECSA na RCSI ya kutoa mafunzo bora kwa
lengo la kuimarisha afya za wanadamu.
Akizungumza
kwenye tukio hilo Rais wa COSECSA , Profesa Stephen Ogendo alisema
kwamba kuwepo kwa maabara hiyo kutasababisha mabadiliko makubwa katika
utoaji mafunzo katika ukanda wa Afrika Mashariki, kati na Kusini (
ECSA).
Alisema
kwamba kutokana na uasili wa maabara hiyo wanafunzi hawatakuwa
wanalazimika kufuata kituo cha mafunzo na badala yake kituo hicho
kitawafuata pale walipo.
Aidha alisema kwamba muundo na mfumo wa ufundishaji umeshatengenezwa kwa ajili ya kusaidia mafunzo hayo kwa nchi wanachama.
Naye
Mkurugenzi wa ECSA anayeshughulikia Afya ya jamii Prof Yoswa Dambisya
alisema kwamba wataendelea kuwa mstari wa mbele kufundisha wataalamu wa
afya kwa kutumia mbinu mbalimbali za kisasa na zenye kutoa tija kama
kuwepo kwa mabara hiyo.
Alisema
kutokana na haja kubwa ya wataalamu wa upasuaji kuwepo kwa maabara hiyo
itembeayo kutasaidia kufunza wanafunzi wengi katika eneo ambalo uwiano
wa wataalamu na wagonjwa ni mtaalamu mmoja kwa wagonjwa 190,000
ukilinganisha na Uingereza ambako uwiano ni mtaalamu mmoja kwa wagonjwa
2,800.
Alisema raslimali kama ya maabara itasaidia kufunza watu wengi zaidi ili kuendelea kupunguza pengo la wataalamu wa upasuaji.
Alisema pia kwamba takwimu za dunia zinaonesha kuwa asilimia 6.5 ya magonjwa yanatokana na kukosekana kwa huduma za upasuaji.
Alisema vifo vingi vinatokana na kukosekana kwa huduma za upasuaji kuliko Malaria, Ukimwi na kifua kikuu kwa pamoja.
COSECSA
ambayo ilianzishwa mwaka 1999 kwa malengo ya kutoa elimu ya upasuaji
ilianzishwa na shirikisho la wapasuaji Afrika Mashariki ambalo lina
miaka takaribani 60.
Wageni mbalimbali wakiangalia namna maabara hiyo inavyofanyakazi.
Mganga
Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa jamiii, Dk. Magreth Mhando (kulia)
akishuhudia zoezi la upasuaji kwa vitendo ndani ya maabara hiyo.
Rais
wa COSECSA , Profesa Stephen Ogendo akizungumza na vyombo vya habari
mara baada ya kukagua maabara hiyo katika uzinduzi huo.
Picha ya pamoja baada ya uzinduzi.
Maabara ya upasuaji ya mafunzo inayotembea iliyotolewa kwa chuo kitembeacho cha COSECSA na serikali ya Ireland.
0 comments:
Post a Comment