Serikali ya Ugiriki imetangaza kuwa benki nchini humo zitafungwa kwa wiki nzima hadi tarehe sita mwezi ujao na itadhibiti kiwango cha fedha zinazotolewa kutoka mashine za benki hatua inayolenga kudhibiti masoko nchini humo ili kuulinda mfumo wa fedha unaoporomoka.
Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras amesema benki zitafungwa kuanzia leo na raia wataruhusiwa kutoa euro sitini pekee kwa siku kutoka kwa mashine za kutoa fedha. Watalii walioko Ugiriki hata hivyo hawataathirika na hatua hiyo.
Nchi kadhaa za Umoja wa Ulaya zimewashauri raia wao waliopo Ugiriki au wanaopanga kuizuru nchi hiyo kuwa na fedha za kutosha.
Hayo yanakuja baada ya Ugiriki na wakopeshaji wake kushindwa kufikia makubaliano muhimu ya kiuchumi mwishoni mwa juma na kupelekea Ugiriki kunyimwa mkopo wa uokozi inayohitaji kwa dharura na hivyo kutishia nchi hiyo kushindwa kulipa madeni yake ifikapo kesho.
Serikali imeitisha kura ya maoni kuamua mustakabali wa nchi hiyo kuhusu mgogoro huo wa kiuchumi.
0 comments:
Post a Comment