Umoja wa Afrika wajitenga na chaguzi za Burundi

04:01 by Kwetuhouse Media


Umoja wa Afrika umetangaza hautatuma waangalizi wake katika chaguzi za bunge na za serikali za mitaa nchini Burundi zinazotarajiwa kufanyika hii leo. 

Taarifa kutoka kwa Umoja huo imesema mazingira nchini Burundi hayako sawa kuweza kuhakikisha chaguzi huru na za haki zinafanyika baada ya wiki kadhaa za ghasia.

Hayo yanakuja muda mfupi baada ya spika wa bunge la Burundi Pie Ntavyohanyuma kutoroka nchini humo na kuitaja azma ya Rais Pierre Nkurunziza kugombea muhula wa tatu kuwa kinyume na sheria. 

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ambaye ametoa wito chaguzi hizo ziahirishwe ameihimiza serikali ya Burundi kuhakikisha chaguzi zinafanyika katika mazingira salama na kuongeza anatiwa wasiwasi na kusisitiza kwa serikali hiyo kuendelea na chaguzi licha ya hali tete ya kisiasa na kiusalama nchini humo. 

Umoja wa Ulaya mwezi uliopita ulisema hautatuma waangalizi katika chaguzi hizo za Burundi.

0 comments:

Post a Comment