AU yataka kuachiwa huru Karenzi Karake
22:30 by Kwetuhouse Media
Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limetaka kuachiwa huru na bila ya masharti yoyote Mkuu wa Idara ya Upelelezi ya Rwanda Jenerali Karenzi Karake anayeshikiliwa nchini Uingereza.
Takwa hilo limetolewa na Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika baada ya mazungumzo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Louise Mushikiwabo na maafisa wa umoja huo mjini Addis Ababa.
Katika mazungumzo hayo Waziri Mushikiwabo ametahadharisha kuhusu utumiaji mbaya wa sheria za kimataifa na vitisho vinavyotokana na hatari hiyo kwa bara la Afrika.
Mahakama ya mwanzo ya Westminster nchini Uingereza Alkhamisi iliyopita ilimuachia Mkuu wa Idara ya Upelelezi ya Rwanda kwa dhamana ya dola milioni moja na laki sita. Karenzi Karake anashikiliwa na mahakama hiyo kwa tuhuma za kuhusika na jinai za kivita. Karake alitiwa nguvuni Jumamosi iliyopita katika uwanja wa ndege wa Heathrow jijini London.
Rais Paul Kagame wa Rwanda amekosoa kitendo hicho akisema kuwa kinaidhalilisha nchi yake. Kagame alisema kuwa watu weusi wanakumbwa na ukandamizaji na ukatili katika nchi za Kimagharibi kutokana na rangi yao.
0 comments:
Post a Comment