Hakimu Mwakalinga siku
alipohukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa mauaji ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Wilaya ya Rungwe. Leo amehukumiwa tena kunyongwa mpaka kufa
katika mauaji ya mlemavu wa ngozi Henry Mwakajila.
MAHAKAMA Kuu Kanda ya
Mbeya leo hii imewahukumu kunyongwa mpaka kufa watu wanne kati ya watano
waliomuua Henry Mwakajila (17) ambaye ni mlemavu wa ngozi (albino).
Waliohukumiwa kunyongwa
mpaka kufa ni Asangalwisye Kayuni maarufu kama Katiti au Mwakatoga na Gerard
Korosso Kalonge (wakazi wa Kijiji cha Mbembati wilayani Ileje), na Leonard
Msalage Mwakisole na Hakimu Mselem Mwakalinga (wakazi wa Kiwira wilayani
Rungwe).
Mshtakiwa wa nne,
Mawazo Philemon Figomole, ameachiliwa huru na mahakama hiyo baada ya ushahidi
wa upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha pasi na shaka kwamba alihusika
katika mauaji hayo.
Akisoma hukumu ya kesi
hiyo ya mauaji yenye kumbukumbu Namb. KIW/IR/49/2008 na PI 5/2013, Jaji wa
Mahakama Kuu Dk. Revila, amesema mahakama imejiridhisha pasi na shaka na
ushahidi wa upande wa mashtaka kwamba washtakiwa hao wanne walitenda kosa hilo
na hivyo wanastahili adhabu hiyo.
Hii ni kesi ya saba ya
mauaji ya albino kutolewa hukumu ambapo mpaka sasa jumla ya watuhumiwa 15
wamehukumiwa kunyongwa mpaka kufa. Ililezwa mahakamani hapo kwamba, mnamo
Februari 5, 2008 majira ya saa 12:00 na saa 1:00 jioni huko katika Kijiji cha
Ilolo, Kata ya Kiwira, tarafa ya Ukukwe, wilayani Rungwe katika Mkoa wa Mbeya,
washtakiwa hao walimteka nyara kijana Henry Mwakajila, ambaye ni mlemavu wa
ngozi aliyekuwa akisoma kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Ukukwe na
kisha kumuua.
Wakati wa mwenendo wa
kesi, ilielezwa na mashahidi wa upande wa mashtaka kwamba mshtakiwa wa kwanza
Asangalwisye Kayuni maarufu kama Katiti au Mwakatoga ambaye ni mganga wa jadi,
mkazi wa Kijiji cha Mbembati, Wilaya ya Ileje, alikutwa na utumbo unaodhaniwa
kuwa wa binadamu na ulipopelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ukathibitika
kwamba ni utumbo wa marehemu Henry.(VICTOR)
Mshtakiwa wa pili,
Gerard Korosso Kalonge wa Kijiji cha Mbembati wilayani Ileje alikutwa na vidole
vinne na mifupa kumi (10) vyote vinavyodhaniwa kuwa vya binadamu na baada ya
uchunguzi wa Mkemia Mkuu wa Serikali ilibainika kwamba ni viungo vya marehemu
Henry Mwakajila.
Ilielezwa pia kwamba,
washtakiwa Leonard Msalage Mwakisole, Mawazo Philemon Figomole na Hakimu Mselem
Mwakalinga ndio waliodaiwa kumteka nyara mtoto huyo na kumuua, kisha kupeleka
viungo kwa mganga wa kienyeji Asangalwisye Kayuni.
Mshtakiwa wa tano,
Hakimu Mselem Mwakalinga, tayari alikwishahukumiwa kunyongwa katika kesi
nyingine ya mauaji ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, John
Mwankenja, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi nyumbani kwake. Hukumu ya kesi
hiyo namba 131/2012 ilitolewa Novemba 13, 2013 ambapo inaelezwa kwamba
watuhumiwa walitenda kosa hilo Mei 19, 2011 katika kijiji cha Mpandapanda, Kata
ya Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya.
Ingawa watuhumiwa
walikuwa wanne, lakini Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya chini ya Jaji Samwel Karua
iliwahukumu kunyongwa mpaka kufa mshtakiwa wa kwanza Hakimu Mwakalinga na
mshtakiwa wa pili Daudi Mwasipasa kwa maelezo kwamba walihusika moja kwa moja
na mauaji hayo ya kukusudia.
Mshtakiwa namba tatu
Obote Mwanyingili yeye alitiwa hatiani kutokana na kosa la kumhifadhi mtuhumiwa
namba moja baada ya kutoka kufanya mauaji wakati mshtakiwa namba nne Kelvin
Myovela alitiwa hatiani kutokana na kuhifadhi silaha iliyotumika katika mauaji
hayo ingawa hakusika na kitendo hicho moja kwa moja, hivyo wote wawili
walihukumiwa kifungo cha miaka saba jela.
Hata hivyo, Myovela
tayari alikwishahukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kukutwa na silaha
kinyume cha sheria.
Inadaiwa kwamba, chanzo
cha mauaji hayo ya John Mwankenja, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha
Mapinduzi Wilaya ya Rungwe, kilitokana na kiongozi huyo kufahamu kwamba hao ndio
waliomuua mlemavu wa ngozi Henry Mwakajila, hivyo aliuawa ili kupoteza ushahidi
0 comments:
Post a Comment