Mwaka 2015 ni mwaka
muhimu katika nchi yetu. Kama ilivyokuwa mwaka 2005 na mwaka 1995 na mwaka 1985
tutakuwa tunapata awamu Mpya ya uongozi.
Chama chetu cha ACT
Wazalendo kitakuwa kinashiriki uchaguzi kwa mara ya kwanza na tutapenda kuwa na
wagombea wenye mwono Mpya kuhusu nchi yetu.
Tunataka kutengeneza
kada ya wanasiasa wenye mwono chanya kuhusu nchi yetu na wenye kuweza kupambana
na ufisadi. Tumekuwa tukisema siku zote kuwa mwarobaini wa ufisadi kwenye kada
ya wanasiasa ni Miiko ya Viongozi.
Miiko itamke wazi kwamba kila kiongozi wa umma
ni lazima atangaze Mali, Madeni na maslahi yake ya kibiashara akiingia kwenye
uongozi na akiwa anatoka. Pia Miiko imzuie Kiongozi kuendesha biashara zake
akiwa katika nafasi ya uongozi. Kwa njia hii uongozi wa umma utakuwa ni kwa
wale tu wanaotaka kutumikia umma na tutazuia watu wanaotaka kujilimbikizia
Mali.
Kutangaza Mali, Madeni na Maslahi pia ni lazima kuendane na uchunguzi wa kuthibitisha matangazo hayo kama ni ya kweli. Hivyo Tume ya maadili ya viongozi lazima iwe na nguvu ya uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya viongozi wa umma watakaosema uwongo au hata kuficha maslahi mbali mbali ambayo umma unapaswa kujua.
Kwa mfano kipindi hiki watu wanatangaza kugombea nafasi ya juu kabisa ya nchi yetu tungeweza kwenda kwenye rekodi za wanaotangaza nia na kutazama maslahi yao ili kujua watu hawa watalinda maslahi gani. Kumekuwa na minong'ono ya dhahiri na ya chini chini dhidi ya watu wanaogombea Urais ambayo lazima wahusika waitolee Maelezo ili wananchi waweze kupembua pumba na Mchele. Mifano michache;
1) Edward Lowasa hanabudi kuwaeleza Watanzania kwa ufasaha kuhusu tuhuma zake katika mchakato wa manunuzi ya kampuni ya kufua Umeme ya Richmond. Mradi huu wa dola 172 milioni ndio uliopelekea yeye kujiuzulu Uwaziri Mkuu. Ndio anasema aliwajibika kwa makosa ya waliochini yake lakini anataka nafasi kubwa sana na yenye nguvu kubwa.
Hivyo bila kuelezea
uhusika wake katika suala hili wananchi wa Tanzania hawatatendewa haki kuuziwa
mbuzi kwenye gunia. Pia ametamka kuwa yeye ni tajiri na anachukia umasikini
lakini hajaeleza utajiri huo ameupataje, ana miliki Mali kiasi gani na ana hisa
kwenye kampuni zipi
2) Prof. Mark Mwandosya
aliwahi kuwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi wakati wa uongozi wa Rais
Benjamin Mkapa. Mashirika yote ya Umma , takribani, katika Wizara hii
yaliyobinafsishwa zoezi la ubinafsishaji liligubikwa na tuhuma za ufisadi na
hata kuchukuliwa upya na Serikali.
Shirika la Ndege la
Taifa lilibinafsishwa chini ya Mwandosya na likafa. Kitengo cha makontena
katika Bandari ya Dar Es Salaam kilibinafsishwa kipindi hiki na kuleta maneno
mengi sana.
Mchakato wa
kubinafsisha Shirika la Reli pia ulianza kipindi hiki. Ubinafsishaji ulioleta
maneno mengi zaidi ulikuwa ni wa Kampuni ya simu ( TTCL) kwa MSI detecon na
Celtel International.
Prof. Mwandosya binafsi alipata tuhuma na
mtoto wake kusomeshwa na watu waliouziwa kampuni hii kwa bei ya chee. Masuala
haya yaliandikwa na vyombo vya habari miaka ya kati ya 2001 na 2005. Prof. Hana
budi kufafanua haya mbele ya umma ili kujiridhisha na uwezo wake wa kupambana
na rushwa na ufisadi.
3) John Pombe Magufuli
anasifika katika uchapa kazi ingawa hajawahi kuonekana waziwazi kwenye
mapambano dhidi ya rushwa. Kwenye kashfa nyingi zilizopata kutokea nchini
msimamo wa Magufuli haujulikani alisimama upande upi.
Wananchi wana haki ya
kupata majibu kutoka kwa Bwana Magufuli kuhusu uuzwaji wa nyumba za Serikali.
Uporaji mkubwa zaidi wa Mali za nchi kuwahi kutokea katika nchi yetu ni uuzwaji
wa nyumba za Serikali.
Waziri Magufuli
alituhumiwa kwa kuuza nyumba kifisadi kiasi cha hata wadogo zake na watu
wengine wasio watumishi wa umma. Wananchi lazima wapate majibu ya mambo haya.
4) Benard Camilius Membe amekuwa akijaribu kuzungumzia ufisadi na nia yake ya kupambana na ufisadi kila apatapo nafasi ya kuzungumza. Hata hivyo anapaswa kuelezea tuhuma dhidi yake kuhusu fedha zaidi ya dola za marekani 20 milioni za mkopo uliorekebishwa kutoka Libya.
Suala hili limekuwa
likisemwa chini chini na hivyo membe mwenyewe kulipotezea lakini ni jambo lenye
kuhitaji Maelezo ya kina kabisa. Msaada huu ulikuwa uwekezwe kwenye kiwanda cha
Simenti mkoani lindi ili kuongeza uzalishaji wa simenti nchini na kuongeza
ajira kwa Watanzania.
Je kiwanda kimejengwa?
Je ndugu Membe anahusika vipi na tuhuma hizi kuhusu fedha za Libya?
Mifano hii ya wagombea
4 wa CCM inaonyesha dhahiri kwamba nchi yetu inahitaji kuelekeza vita dhidi ya
ufisadi kwa kujenga taasisi imara na madhubuti za uwajibikaji.
Vinginevyo vita dhidi
ya rushwa na ufisadi inakua ni porojo tu za wanasiasa. Wote tuliowainisha hapo
juu wamesema katika hotuba zao za kutia nia kuwa watambana na rushwa. Hakuna
aliyesema atapambana vipi na rushwa na ufisadi. Hakuna aliyethubutu kutamka
neno Miiko ya Viongozi.
Hakuna aliyethubutu kusema ataweka wazi Mali,
Madeni na Maslahi yake.
Hata wagombea wa kambi ya upinzani wanatamka kupambana na rushwa lakini hawatamki namna gani watambana na rushwa. Nao pia wanaona aibu kuzungumzia Miiko ya Viongozi.
Hata wagombea wa kambi ya upinzani wanatamka kupambana na rushwa lakini hawatamki namna gani watambana na rushwa. Nao pia wanaona aibu kuzungumzia Miiko ya Viongozi.
Sisi ACT Wazalendo
lazima tuwe tofauti kwa kuteua mgombea Urais ambaye ataweka ajenda ya Miiko
kama ajenda kuu na tuseme hivyo waziwazi bila kumung'unya maneno. Hii ndio
itakuwa tofauti yetu na vyama vikongwe.
Ufisadi hauondolewi kwa
maneno matupu. Siasa Mpya ni siasa za uwazi na uwajibikaji. Ni siasa za Miiko
ya Viongozi kama ilivyoainishwa kwenye Azimio la Tabora linalohuisha Azimio la
Arusha.
0 comments:
Post a Comment