Kificho ajivunia kufaulu Mithani.

22:39 by Kwetuhouse Media


 SPIKA wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho amewaaga wajumbe wa baraza hilo na kusema amefaulu mtihani mkubwa uliokuwa ukimkabili kuliongoza Baraza la Wawakilishi likiwa katika muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa mafanikio makubwa.


Kificho alisema hayo wakati akiwaaga wajumbe hao kutokana na kumalizika kwa uhai wa baraza la wawakilishi kipindi cha miaka mitano sasa.

Alisema amefaulu mtihani mkubwa uliokuwa ukimkabili wa kuliongoza baraza la wawakilishi likiwa na muundo wa Serikali ya umoja wa kitaifa kwa mafanikio makubwa kutokana na ushirikiano waliompatia wawakilishi wote wakiongozwa na mawaziri.
Alisema Baraza la Wawakilishi liliendeshwa kama vile wajumbe wote wa baraza hilo wanatoka katika chama kimoja huku wakitetea hoja moja.

“Miongoni mwa mafanikio makubwa ambayo leo hii najivunia ni kuwa spika wa kwanza kuliongoza baraza la wawakilishi likiwa katika muundo wa serikali ya umoja wa kitaifa kama ni moja ya mtihani mkubwa uliokuwa ukinikabili,”alisema.

Alisema, “watu wengi ikiwemo viongozi wa nchi washirika wa maendeleo walikuwa wanajiuliza jinsi tutakavyoiongoza serikali ya umoja wa kitaifa kwa mafanikio makubwa, lakini kwa bahati nzuri tumeweza”.

Aidha Kificho aliwapongeza wajumbe hao na kusema hakuna jambo lililomkwaza katika kipindi cha miaka mitano akiwa Spika wa Baraza la Wawakilishi katika Serikali yenye muundo wa umoja wa kitaifa kutoka kwa wajumbe wa baraza hilo ambalo linaundwa na wajumbe kutoka katika vyama viwili vya sasa CCM na CUF.

“Hakuna jambo ambalo limenikwaza kwenu nyinyi wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, lakini pia kama kuna jambo nimewakwaza basi naomba mnisamehe ndiyo hulka na tabia ya binadamu kukosea kwani sisi sio wakamilifu hata kidogo,” alisema.

Kificho alisema Wawakilishi wamefanikiwa kutekeleza majukumu yao ambayo ni kuwatetea wananchi kwa ajili ya kupata maendeleo katika majimbo ya uchaguzi.

Alisema kazi hiyo imefanyika vizuri ambapo mara nyingi mawaziri wamekuwa wakisikiliza mahitaji na kutekeleza ahadi za wajumbe katika majimbo ya uchaguzi.

Kificho aliwapongeza wasaidizi wake akiwemo naibu spika wa baraza la wawakilishi, Ali Abdalla Ali pamoja na wenyeviti wa baraza hilo kwa utendaji kazi wenye kuzingatia maadili ya shughuli za baraza la wawakilishi.

Alimpongeza Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi, Mgeni Hassan Juma kwa utendaji wake ambao umefanikisha kusimama kwa jumuiya ya umoja wa wanawake wa Baraza la Wawakilishi (Uwawazi) na kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

HABARI LEO.

0 comments:

Post a Comment