Kada wa CCM, Helena Elinawinga akionyesha begi lenye fomu za kuomba
kugombea kiti cha Urais kupitia chama cha CCM, baada ya kukabidhiwa jana
katika makao makuu ya chama hicho, mjini Dodoma. Picha na Edwin Mjwahuzi
Dodoma/Dar. Mtafiti
binafsi na kada wa CCM, Helena Elinawinga (41), amejitokeza kuchukua fomu ya
kuomba kuteuliwa na chama chake kuwania urais na kusema amefikia uamuzi huo ili
kupunguza kujirudiarudia kwa adhabu za vifo kwa viongozi.
Helena anakuwa kada wa
40 wa CCM kuomba ridhaa ya chama hicho kuteuliwa kupeperusha bendera yake
katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Kada huyo ni mwanamke
wa sita kuchukua fomu za kuomba kuwania nafasi hiyo katika chama hicho
akitanguliwa na Balozi Amina Salum Ali, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa
Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk Mwele Malecela, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk
Asha-Rose Migiro, Monica Mbega na Ritta Ngowi.
Helena alifika katika
ofisi za Makao Makuu ya CCM saa saba mchana akiwa ndani ya bajaji lakini
tofauti na wenzake, akiwa amevalia shati la rangi ya zambarau, suruali nyeusi
na kofia yenye rangi za Taifa.
Akiwa na Katibu wa
Oganaizesheni, Muhammed Seif Khatib, kada huyo ambaye pia hakuwa na wapambe
kama ilivyo kwa wagombea wengine, alikataa ombi la wapigapicha kuvua kofia.
“...nitawaambia kitu kizuri baadaye kwa nini sitaki kuvua hii kofia,” alisema
huku Khatib akiwasihi waandishi kutoendelea kumtaka avue au asogeze kofia hadi
atakapomaliza kuchukua fomu.
Aidha, wakati
akichukua fomu hiyo, kada huyo ambaye mkononi alikuwa amebeba begi
lililotengenezwa kwa kitambaa cha nguo aina ya batiki, alilazimisha kupigwa
picha pamoja na bango lake huku akisisitiza umuhimu wa picha hiyo kupigwa hata
kabla ya kumaliza shughuli ya kukabidhiwa fomu.
Bango hilo, licha ya
kuwa na maneno ambayo yalikuwa hayaeleweki vizuri na michoro ya watu waliovalia
mavazi ya kifalme, moja lilionyesha akiwa amebeba mizani inayotumiwa na
mahakama kuonyesha usawa wa sheria na mkono mwingine akiwa amebeba jambia. Bango
hilo pia lilikuwa na gari aina ya shangingi, picha za marais wa zamani wa
Liberia, Charles Taylor, Mohammed Morsi wa Misri na wanawake wengine wawili
ambao hawakufahamika.
Akizungumza mara baada
ya kukabidhiwa fomu hiyo, huku akicheka, Helena alisema: “Nilikataa kuvua kofia
kwa sababu sikuchana nywele.”
Kuhusu kutovaa sare za
CCM, Helena alisema aliwaambia viongozi wa chama chake kuwa wanatakiwa kufanya
mafunzo ya pamoja ya wagombea wote ili kuelewa hadhi ya sare. Alipoulizwa kama
siku saba zitamtosha kukusanya wadhamini katika mikoa 15 alisema; “Huwezi kujua
nini kitatokea kama utakuwa hai au utakufa.”
Helena ni nani?
Alizaliwa Desemba 31
mwaka 1974, Dar es Salaam na kusoma shule tatu za msingi tofauti mkoani Arusha
na Kilimanjaro. Alijiunga na Shule ya Sekondari Weruweru ya Kilimanjaro na
baadaye Chuo Kikuu cha Marekani katika Shule ya Masomo ya Kimataifa na
kutunukiwa Shahada ya Siasa ya Mazingira na Uchumi.
Hivi sasa anafanya
utafiti wa jinsi vijana wanavyoweza kujiajiri wakimaliza vyuo akishirikiana na
Chuo cha Mwalimu Nyerere Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Sokoine Morogoro.
Lowassa avunja rekodi
ya Mbeya
Zaidi ya wana CCM
120,000 walijitokeza juzi kumdhamini Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
jijini Arusha na kuvunja rekodi ya Mkoa wa Mbeya alikodhaminiwa na zaidi ya
wanachama 58,000.
Shughuli ya kumdhamini
Lowassa zilizofanyika katika Viwanja vya Msikiti Mkuu wa Ijumaa (zamani bustani
ya Mashujaa), ilimalizika saa 10.47 jioni, licha ya maandalizi yake kuanza
tangu saa nne asubuhi kwa burudani za nyimbo za hamasa za CCM. Lowassa
aliwasili uwanjani hapo Saa 10.07 jioni.
Muhongo, Mulenda
wamaliza kazi
Waziri wa zamani wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amerejesha fomu ya kuomba kuteuliwa
kuwania urais na kutaka wanaomhusisha na sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow,
kuhojiwa kama tatizo ni urais.
Akizungumza jana baada
ya kurejesha fomu, Profesa Muhongo alisema hana haja ya kuzisemea tuhuma hizo
kwa kuwa hakuna chombo ambacho kimemtaja kuhusika.
“Waliokuwa wamelisuka
waende walitolee maelezo. Ripoti ya CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali) jina langu halipo,” alisema Profesa Muhongo.
Aliwataka Watanzania
kusoma taarifa za mabenki ambazo zinaonyesha watu waliogawana fedha hizo na
kwamba jina lake halipo. “Sikuitwa na Kamati ya Maadili ya Viongozi wa Umma,
sasa nizungumzie nini? Takukuru sikuitwa nieleze nini?” alihoji.
Katika makabidhiano
hayo, Profesa Muhongo pia alimkabidhi Khatib CD 15 zenye orodha ya wadhamini,
picha na maoni ya kila mdhamini katika mikoa yote.
Pia, alikabidhi ramani
ya maeneo aliyozunguka kusaka wadhamini.
Alisema Watanzania
hawatafuti mtu wa kujaza nafasi ya urais ila ambaye anaweza kufanya mapinduzi
yatakayowatoa katika umaskini na kwamba mtu sahihi ni yeye.
Aidha, Mwenyekiti wa
shirika lisilo la kiserikali la Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Jamii (EGSOF),
Leonce Mulenda, amerudisha fomu na kusema amepokewa vyema katika mikoa yote
aliyokwenda kutafuta wadhamini.
Makongoro amkubali
Profesa Lipumba
Mbunge wa Bunge la
Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere ameunga mkono kauli iliyotolewa na
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akisema baadhi ya wagombea wenzake
hawapaswi kuwa kwenye kinyang’anyiro hicho kwa vile siyo wasafi na wangetupwa
jela kutumikia vifungo.
Juni 14 mwaka huu,
Profesa Lipumba, wakati akichukua fomu kuwania urais kupitia CUF ili
apendekezwe na Ukawa, alionyesha kushangazwa na utitiri wa wagombea ndani ya
CCM akisema baadhi yao walipaswa kuwa gerezani wakitumikia kifungo kutokana na
kuhusika katika kashfa mbalimbali za ufisadi.
Akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam jana baada ya kumaliza kazi ya kukusanya
wadhamini, Makongoro alisema kuwa kamwe hawezi kuwa rafiki na mafisadi.
Alisema walarushwa na
mafisadi katika CCM ndio wanaofanya baadhi ya wanachama wa chama hicho wenye
sifa, kukosa nafasi za uongozi.
“Mimi siyo mnafiki,
naungana na kauli hii aliyoitoa kaka yangu Ibra... si mnamjua Ibra...?” alisema
Makongoro.
Dk Mwele azoa wanawake
Wanawake jijini Dar es
Salaam wamejitokeza kwa wingi kumdhamini Dk Mwele Malecela, anayeomba kuteuliwa
na CCM kuwania urais.
Katibu wa CCM Wilaya
ya Temeke, Robert Kerenge alisema mgombea huyo ni wa 11 kuomba udhamini katika
ofisi yake, lakini alishangaa kuona idadi kubwa ya wanachama waliojitokeza
kumdhamini tofauti na ilivyokuwa kwa wagombea wengine.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment