HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR,
MHE. BALOZI SEIF ALI IDDI
KATIKA UFUNGAJI
WA MKUTANO WA 20 WA BARAZA
LA WAWAKILISHI
ZANZIBAR, TAREHE 30 JUNI,
2015
--------------------------
1.0 Mheshimiwa
Spika, sina budi kuanza hotuba yangu hii kwa kumshukuruMwenyezi
Mungu Mtukufu Mwingi wa Rehema kwa kutujaalia uhai uzima, afya njema na
kutuwezesha kumaliza Mkutano huu wa 20 wa Baraza la
Wawakilishi la Nane kwa mafanikio makubwa. Aidha, nachukua nafasi hii
kukupongeza na kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika, kwa umahiri na umakini
wako mkubwa wa kuliendesha Baraza hili Tukufu kwa kipindi chote cha
Uongozi wako. Sisi sote ni mashahidi wa namna ulivyodhihirisha uwezo na
uzoefu wako wa kuliongoza Baraza hili katika kuisimamia na kuishauri
Serikali juu ya utekelezaji wa mipango mbali mbali ya kuwaletea
wananchi wetu maendeleo. Kwa kweli umetuongoza vizuri. Pia, napenda
kumshukuru Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na Waheshimiwa Wenyeviti wote wa
Baraza kwa kukusaidia ipasavyo katika kuviendesha vikao vya Baraza hili.
2.0 Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa shukrani za pekee pamoja na kumpongeza
kwa dhati kabisa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa uongozi wake uliojaa hekima na busara
kubwa ambao umeiwezesha nchi yetu kuzikabili changamoto za kiuchumi
na kisiasa na kupiga hatua za kimaendeleo. Aidha, napenda kuchukua fursa
hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa imani yake kwangu ya kuniteua kushika
nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais katika kipindi cha kwanza cha Serikali ya
Awamu ya Saba chini ya uongozi wake.
3.0 Mheshimiwa
Spika, vile vile napenda kumshukuru sana Makamu wa Kwanza
wa Rais Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad kwa kumsaidia na kumshauri
Mheshimiwa Rais katika kuiongoza nchi yetu. Aidha, namshukuru Mheshimiwa Makamu
wa Kwanza wa Rais kwa mashirikiano yake makubwa kwangu binafsi na kwa Ofisi
yangu katika kutekeleza mipango na malengo yaliyowekwa na Serikali.
Hakika katika kipindi hiki cha miaka mitano, Serikali ya kwanza yenye mfumo wa
Umoja wa Kitaifa imefanya kazi nzuri sana ya kuiletea nchi yetu maendeleo.
4.0 Mheshimiwa
Spika, nachukua
fursa hii pia kuwashukuru na kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri
kwa kuwasilisha bajeti za Wizara zao na kujibu vizuri na kwa umakini mkubwa
hoja mbali mbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wawakilishi. Ni matumaini yangu kwamba, Waheshimiwa Wajumbe
na wananchi waliokuwa wakifuatilia kwa karibu zaidi mijadala ya mkutano huu
wamefaidika na majibu na ufafanuzi uliotolewa. Vile vile, nawashukuru na
kuwapongeza sana Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza lako Tukufu kwamichango, mapendekezo na ushauri wao
waliotoa wakati wa kuzijadili
Hotuba za Bajeti zilizowasilishwa hapa Barazani. Nawashukuru Wajumbe wote
kwa kuzipitisha bajeti hizo bila ya pingamizi zozote. Kwa kweli katika
mikutano yote ya Baraza lako tukufu, mkutano huu ulikuwa wa kupigiwa mfano kwa
kupitisha bajeti zote kwa urahisi. Upitishaji wa bajeti hizo ulikuwa
rahisi zaidi kwa sababu ya kutumia mfumo mpya wa bajeti ulioitwa “Program Based
Budget” (PBB). Buti hazikuwa nyingi mara hii ukifananisha na bajeti
zilizopita. Nawashukuru sana Wajumbe kwa ushirikiano wao.
5.0 Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa naomba kuchukuwa fursa hii kuwakumbuka
wenzetu waliokwishafika mbele ya haki ambao walikuwa Wajumbe wa Baraza
hili. Wajumbe hao ambao wametutoka katika kipindi cha miaka mitano (5)
hii ni Marehemu Mussa Khamis Silima aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Uzini
ambae alifariki tarehe 23 Agosti, 2011, Marehemu Salum Amour Mtondoo aliyekuwa
Mwakilishi wa Jimbo la Bububu ambae alifariki tarehe 15 Machi, 2012, Marehemu
Salmin Awadh Salmin aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni aliyefariki
tarehe 19 Februari, 2015 na Marehemu Ali Khamis Abdalla aliyekuwa Spika Mstaafu
alifariki tarehe 8 Agosti, 2014. Viongozi hao walikua mahodari, wenye
msimamo thabit, makini na shupavu na walijitolea kwa hali na mali katika
kuwatumikia wananchi kwa kipindi chote cha uhai wao. Hatuna budi kuyaenzi na
kuyaendeleza yale yote mema ambayo wenzetu hao wametuachia kwa manufaa ya nchi
yetu. Kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar naendelea kuwapa pole
Waheshimiwa Wajumbe, wanafamilia na wananchi wote kwa ujumla kwa misiba hii.
Sisi sote ni waja wake Mwenyezi Mungu na bila ya shaka marejeo yetu ni
kwake. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahala pema peponi.
Amin.
6.0 Mheshimiwa Spika, kama tunavyoelewa kwamba Mkutano huu wa 20 ni mkutano wa mwisho
kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu hapo tarehe 25 Oktoba, 2015. Hivyo, natoa
shukurani za dhati kwako wewe Mheshimiwa Spika, viongozi wote na wafanyakazi wa
Baraza kwa mashirikiano makubwa katika kuliendesha Baraza katika kipindi chote
cha miaka mitano (5). Nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri,
Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na Wakuu wa Mashirika yote ya Umma kwa bidii na
juhudi kubwa katika kutekeleza majukumu yao waliyopangiwa. Jambo ambalo
limechangia sana katika hatua za maendeleo tuliyopata katika nchi yetu.
Nawashukuru wananchi wote wa Zanzibar kwa utulivu wao na mashirikiano yao na
Serikali katika harakati za kuiletea maendeleo nchi yetu. Ni imani yangu
kwamba, wananchi wote wataendelea kuiamini na kuiunga mkono Serikali yao
inayoongozwa na Rais kutoka CCM, na watashiriki katika harakati za Uchaguzi
Mkuu ujao kwa upendo, amani na utulivu uliokwisha jengeka miongoni mwa jamii
yetu.
7.0 Mheshimiwa
Spika, mafanikio tuliyoyapata katika Kipindi cha Kwanza cha Awamu ya Saba
katika Sekta mbali mbali ikiwemo Sekta ya Afya, Elimu, Utalii, Maji na
Miundombinu na Mawasiliano na katika Sekta za Uzalishaji (viwanda, kilimo,
mifugo na uvuvi) ni ya kupigiwa mfano na tuna kila sababu ya kumpongeza Rais
wetu Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa mafanikio haya makubwa.
Mafanikio haya makubwa yametokana na utekelezaji sahihi wa Ilani ya CCM ya
mwaka 2010 – 2015. Sina shaka kwa mafanikio haya, Rais Shein atarudi tena
kuiongoza Serikali hii yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa.
8.0 Mheshimiwa Spika, kama tunavyojua kwamba Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ni moja
kati ya mihimili mitatu ya nchi yetu ambalo ndilo lenye Mamlaka ya Kutunga
Sheria na Kusimamia Utekelezaji wa Shughuli za Umma kama ilivyoainishwa katika
Kifungu cha 5 A (1) na (2) cha Katiba ya Zanzibar ya 1984.
9.0 Mheshimiwa
Spika, Baraza hili la Nane hadi sasa limeshafanya jumla ya mikutano
20. Katika mikutano hiyo, jumla ya maswali ya msingi 1,630 na maswali ya
nyongeza 3,277 yameulizwa kwa Serikali na kujibiwa. Aidha, Baraza
limefanikiwa kujadili na kupitisha Miswada ya Sheria 63 na hatimaye kutungwa
Sheria kutokana na Miswada hiyo. Pia, Baraza hili limeidhinisha Bajeti ya
Serikali na Mawizara mara tano (5) hadi sasa. Bajeti ambazo zimesaidia
kufanikisha kupatikana kwa maendeleo makubwa nchini mwetu.
10.0 Mheshimiwa
Spika, vile vile, Baraza hili la Nane liliunda jumla ya Kamati Teule
tano (5) ambazo zilikuwa kama zifuatazo:-
a. Kamati Teule ya Kuchunguza Baraza la
Manispaa.
b. Kamati Teule ya Kuchunguza Utendaji wa
Shirika la Umeme (ZECO).
c. Kamati Teule ya Kuchunguza mambo mbali
mbali yaliyoibuka kwenye majadiliano ya Bajeti ya mwaka 2011/2012.
d. Kamati Teule ya Kuchunguza Migogoro ya
Ardhi.
e. Kamati Teule ya Kuchunguza Upotevu wa
Nyaraka.
Ripoti za Kamati Teule zote ziliwasilishwa Serikalini na
kuchukuliwa hatua zilizostahili.
11.0 Mheshimiwa
Spika, Baraza pia lilipokea na kujadili hoja binafsi za Wajumbe kama
ifuatavyo:-
a. Hoja ya Mhe. Hamza Hassan Juma,
Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura, inayohusu Mkopo wa Elimu ya Juu.
b. Hoja ya Mhe. Hija Hassan Hija,
Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani, inayohusu Utendaji wa Shirika la Umeme (ZECO).
c. Hoja ya Mhe. Mgeni Hassan Juma,
Mwakilishi Viti Maalum, inayohusiana na vitendo vya Udhalilishaji wa Watoto,
Zanzibar.
d. Hoja ya Mhe. Jaku Hashim Ayoub,
Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni inayohusiana na Uimarishaji wa Huduma za Afya
zinazotolewa kwa wananchi wa Zanzibar, na
e. Hoja ya Mhe. Hamad Masoud Hamad,
Mwakilishi wa Jimbo la Ole inayohusu Ucheleweshaji wa Upatikanaji wa
Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.
Hoja zote hizo zilipokelewa na Baraza lako tukufu, kujadiliwa na
kutolewa maamuzi stahili.
12.0 Mheshimiwa
Spika, moja kati ya mambo makubwa na muhimu yaliyofanyika ndani ya
Baraza hili la Nane ni Wajumbe wa Baraza lako kushiriki katika Bunge Maalum la
Katiba kwa lengo la kuandaa Katiba Inayopendekezwa. Napenda kuchukua fursa hii
kuwapongeza Waheshimiwa Wajumbe wote kwa ushiriki wao uliowezesha kupatikana
kwa Katiba Inayopendekezwa ambayo hivi sasa inasubiri kupigiwa kura ya maoni na
wananchi. Katiba hii inayopendekezwa imesaidia kutatua kero nyingi
zilizokuwa zinalalamikiwa na upande wa Zanzibar. Miongoni mwa kero hizo
ni kutolewa kwa suala la mafuta na gesi asilia kutoka kwenye orodha ya mambo ya
Muungano. Katiba hiyo imelitoa suala la mafuta na gesi asilia kutoka
kwenye orodha hiyo. Kero hiyo ni miongoni mwa kero nyingi zilizokuwa
zinalalamikiwa ambazo tayari zimekwisha patiwa ufumbuzi kupitia Katiba
Inayopendekezwa.
MAFANIKIO YA SERIKALI YA
AWAMU YA SABA:
13.0 Mheshimiwa
Spika, katika kipindi hiki cha Awamu ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa tumeshuhudia maendeleo makubwa ya
kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kwa upande wa kisiasa, Serikali imeweza
kuimarisha umoja wa kitaifa na mshikamano wa wananchi wetu bila ya kujali
itikadi zao za kisiasa. Hali ambayo imepelekea kuimarika kwa uvumilivu wa
kisiasa miongoni mwa viongozi na wanachama wa vyama vya siasa na wananchi kwa
ujumla.
14.0 Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa maendeleo ya kiuchumi, hali ya uchumi wetu
imeimarika kwa kasi na umekua kutoka asilimia 5.2 mwaka 2010 hadi asilimia 7.4
mwaka 2015. Ukuaji huo unatokana na kuimarika kwa sekta ya kilimo,
misitu, uvuvi, viwanda na utalii. Kasi ya mfumko wa bei imepungua kutoka
asilimia 6.1 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 5.6 mwaka 2014. Hali
hii inatokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa ndani unaotokana na juhudi
zilizochukuliwa na Serikali katika kuwapatia ruzuku za pembejeo wakulima
wetu. Katika kipindi hiki cha miaka mitano (2010 – 2015), Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imetoa fidia ya jumla ya Shs. 7,129,591,148 za kuendeleza
kilimo, kwa ajili ya ununuzi wa mbolea, madawa, mbegu na kutoa huduma za
matrekta kwa wakulima.
15.0 Mheshimiwa
Spika, kilimo bado kinaendelea kuwa ni mhimili mkuu wa uchumi wetu na
ndicho kinachotoa ajira kwa wananchi walio wengi, kwa kutambua hilo Serikali
imeweza kutekeleza programu na miradi mbali mbali ya kilimo. Juhudi hizi
zimepelekea kuimarika utoaji wa elimu kwa wakulima wa mazao ya chakula,
biashara, viungo na matunda, matumizi ya pembejeo, matumizi ya zana za kisasa
za kilimo ikiwemo matrekta na miundombinu ya umwagiliaji maji mashambani.
16.0 Mheshimiwa
Spika, Serikali imeendelea kuliimarisha na kuliendeleza zao la karafuu
kwa kuotesha miche na kugaiwa bure kwa wakulima wetu Unguja na Pemba.
Aidha, wakulima wetu wameendelea kupatiwa taaluma ya kilimo bora cha karafuu
ikiwemo uimarishaji wa vitalu vya miche ya mikarafuu, uchanganyaji wa mazao
mengine (mixed cropping), uvunaji na uanikaji bora wa zao hili. Lengo ni
kuhakikisha upatikanaji wa karafuu kwa wingi na zenye viwango vitakavyoipatia
nchi yetu bei nzuri katika soko la dunia, ndiyo maana Serikali inawahamasisha
wakulima kuyaweka mashamba yao ya mikarafuu katika hali ya usafi. Serikali kwa
upande wake inajitahidi kuyaweka mashamba ya Serikali ya mikarafuu katika hali
ya usafi.
17.0 Mheshimiwa
Spika, Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya Bakhressa imeendelea
na juhudi za kumarisha maeneo huru ya kiuchumi ya Fumba. Mpango
ulokuwepo ni kuendeleza eneo la Fumba uwe miongoni mwa miji ya kibiashara
nchini. Kupitia jitihada hizo, ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji na
umeme unaendelea, na kwa kuanzia barabara mbili zenye urefu wa kilomita 4.2
ujenzi umekamilika. Aidha, Kiwanda cha kuzalisha bidhaa zitokanazo
na maziwa kinafanya kazi na kinaendelea kutoa ajira kwa vijana wetu.
18.0 Mheshimiwa
Spika, Sekta ya Utalii imeendelea kuimarika. Idadi ya watalii
walioingia nchini imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka na kufikia
watalii 274,619 mwaka 2015. Ongezeko hili linatokana na kuimarika kwa
miundombinu ya utalii pamoja na hali ya amani na utulivu uliopo nchini.
Nawaomba viongozi na wananchi wote kuendelea kudumisha amani katika nchi yetu
hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu ili utalii wetu uzidi
kuimarika na uchumi wetu uzidi kukua. Serikali inawahakikishia watalii
wetu hao usalama wao kwa kipndi chote ambacho watakuwa nchini mwetu.
Katika kuimarisha zaidi Sekta hii ya
Utalii, Serikali imeamua kuibadilisha mandhar ya Hoteli ya Bwawani, hoteli
ambayo ina historia kubwa baada ya kupatikana mwekezaji ambaye yuko tayari
kuibadilisha hali hiyo. Mazungumzo baina ya Serikali na mwekezaji
yamefikia mbali na sasa bado tu Serikali kumkabidhi mradi huo kwa mwekezaji na
kufunga naye mkataba.
19.0 Mheshimiwa
Spika, Sekta ya Miundombinu nayo imepata mafanikio makubwa ikiwa ni
pamoja na ujenzi wa barabara mpya kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilomita
243.85 kwa Unguja na Pemba. Vile vile barabara zenye urefu wa kilomita 39.3
zimejengwa kwa kiwango cha kifusi. Aidha, barabara zenye urefu wa kilomita 656
zimefanyiwa matengenezo mbali mbali. Ni matumaini yangu kwamba, ujenzi wa
barabara hizi utasaidia ukuaji wa uchumi wa nchi yetu, hivyo napenda
kutoa wito kwa watumiaji wa barabara hizi na wananchi kwa ujumla kuzitunza kwa
faida yetu na vizazi vyetu vijavyo. Wale wenzetu wenye tabia ya kuchoma
barabara hizo kwa makusudi waiache tabia hiyo kwani inaigharimu Serikali fedha
nyingi kuzitengeneza tena barabara hizo. Serikali itawachukulia hatua
kali waharibifu hao.
20.0 Mheshimiwa
Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa Sekta ya Usafiri Baharini
imeendelea kuimarisha usafiri wa baharini kwa kujenga majengo mapya ya
kuhudumia abiria katika bandari ya Malindi Unguja. Aidha, Serikali
imeshanunua meli mpya huko Korea yenye uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na tani
200 za mizigo ambayo inatarajiwa kuwasili mwishoni mwa mwezi wa Julai mwaka
huu. Aidha, Serikali imeendelea kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa
kuendeleza dhamira ya ujenzi wa bandari mpya, kubwa na ya kisasa katika
maeneo ya Mpigaduri ambapo hatua za uchambuzi yakinifu, michoro pamoja na
makubaliano ya ujenzi huo na kampuni ya China Habour Engeneering Companyyamekamilika. Vile vile,
Serikali inaendelea na utaratibu wa kuziendeleza bandari zetu zote za Unguja na
Pemba. Uamuzi wa ujenzi wa bandari ya Mpiga Duri ulifanywa na Serikali ya
Awamu ya Tano kuendelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita, na Serikali ya Awamu ya
Saba ndiyo iliyoendeleza mradi huo kwa kutafuta wafadhili wa kuijenga bandari
hiyo.
Ilani ya CCM ya mwaka 2010 – 2015 kifungu
143 (e) inasema:
“Kusimamia utekelezaji wa Mpango Mkuu
(Master Plan) wa bandari ya Malindi, ikijumuisha huduma za bandari huru na
kuendelea kutafuta uwezo wa kujenga bandari mpya ya kibiashara ya Mpiga
Duri”. Mhe. Rais anafanya kazi kubwa sana kuhakikisha kuwa mradi
unatekelezwa na ndiyo tumefikia hapa tulipo. Mradi huu utaanza kujengwa mara tu
mradi wa Terminal II utakapokamilika. Hivyo, Serikali itakayokuja itauendeleza
tu mradi huu na siyo kuuanzisha.
21.0 Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa usafiri wa anga, Serikali imejenga maegesho
na njia za kupitia ndege katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani
Karume. Vile vile, ujenzi wa jengo jipya la abiria la kiwanja hicho unaendelea
vizuri na unatarajiwa kukamilika mwezi wa Oktoba mwaka huu. Aidha,
Serikali inaendelea na uimarishaji wa Uwanja wa Ndege wa Sheikh Abeid Amani
Karume - Pemba kwa kuuwekea taa na kuufanyia matengenezo katika njia yake ya kurukia
na kutulia ndege. Kukamilika kwa ujenzi huo kutaimarisha utoaji wa huduma za
abiria na mizigo katika viwanja vyetu vyote nchini.
22.0 Mheshimiwa
Spika, mafanikio makubwa yameweza kupatikana katika Sekta ya Elimu
katika ngazi zote kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari na elimu ya
juu. Miongoni mwa mafanikio hayo ni kupunguza tatizo la upungufu wa
walimu, maabara, vitabu vya kiada na ziada pamoja na uhaba wa madarasa na
samani. Aidha, Serikali imefanikiwa kwa asilimia 100 kuwaandikisha
wanafunzi wote waliotarajiwa kuanza darasa la kwanza mwaka 2015.
23.0 Mheshimiwa
Spika, Serikali pia imeendeleza ujenzi wa skuli za sekondari na
kukamilisha ujenzi wa skuli za msingi ambazo zimekuwa zikianzishwa na wananchi
wenyewe katika maeneo mbali mbali ya nchi yetu. Sambamba na mafanikio hayo,
Serikali imeendelea kuwapatia mikopo ya elimu ya juu wanafunzi ili kuwawezesha
kujiunga na vyuo mbali mbali ndani na nje ya nchi. Aidha, Serikali imekuwa
ikishirikiana na Vyuo Vikuu vilivyopo Zanzibar ili kuongeza fani za masomo
kuanzia ngazi ya Shahada ya Kwanza na kuendelea ili kupata wataalamu wa fani
mbali mbali.
24.0 Mheshimiwa
Spika, kupitia Baraza lako Tukufu napenda kutoa wito kwa wananchi
kuendelea kushirikiana na Serikali katika jitihada za ujenzi na usimamizi wa
skuli katika maeneo yao. Aidha, natoa wito kwa wale wote waliopatiwa
mikopo ya elimu ya juu kulipa mikopo hiyo ili kuwawezesha wanafunzi wengine
kupata huduma hiyo.
25.0 Mheshimiwa
Spika, Serikali
inaendelea na juhudi zake za kupambana na magonjwa mbali mbali ya kuambukiza na
yasiyo ya kuambukiza. Zanzibar imekuwa mfano kwa nchi za Afrika Mashariki na
dunia kwa kuweza kutokomeza ugonjwa wa Malaria. Aidha, Serikali inaendelea
kuiimarisha Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa kujenga na kuweka vifaa vya
kisasa ili kuipandisha daraja na kuwa hospitali ya Rufaa na Kwa upande wa
Hospitali za Kivunge, Makunduchi na Chake Chake kuwa Hospitali za
Wilaya. Hospitali za Abdalla Mzee Mkoani na Hospitali ya Wete
zinaimarishwa ili ziweze kupandishwa daraja na kuwa Hospitali za Mkoa.
Katika mwendelezo wa kuimarisha huduma ya afya kwa wananchi wetu, Serikali
imezipatia hospitali vifaa vya kisasa pamoja na usambazaji wa dawa kwa
wananchi. Vile vile Serikali ya Awamu ya Saba kwa kushirikiana na
Washirika wa Maendeleo imeweza kujenga Bohari Kuu ya Dawa ya kisasa ambayo ni
mfano katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.
26.0 Mheshimiwa Spika, UKIMWI na Dawa za Kulevya ni miongoni mwa
matatizo yanayoathiri makundi mbali mbali ya watu, hasa vijana. Katika
suala la UKIMWI, kiwango cha mambukizi kimeendelea kubakia kuwa asilimia 0.6 na
idadi ya watu walioambukizwa virusi vinavyosababisha UKIMWI (VVU) waliosajiliwa
ni 7,820. Kati ya hao watu 5,375 wanapata huduma ya ARV. Katika
kuendeleza mapambano dhidi ya UKIMWI, Serikali imechukuwa hatua mbali mbali,
zikiwemo kuimarisha huduma za tiba, huduma za kuzuia maambukizi ya mama kwenda
kwa mtoto. Aidha, Serikali imesambaza mashine tatu mpya za CD4
ambazo zimepelekwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Mwembeladu, na Kivunge, na
mashine aina mbili za “Haematology” na “Chemistry” zimesambazwa katika
Hospitali za Micheweni, Makunduchi, na Mwembeladu. Pia, Serikali
imeimarisha vituo vya ushauri nasaha na upimaji wa VVU. Vile vile,
Serikali kwa kushirikiana na Taasisi zisizo za Serikali (NGOs) inaendelea na
shughuli za kuelimisha jamii juu ya mapambano dhidi ya UKIMWI na kupunguza
unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU. Pia, vituo vinavyotoa huduma ya ushauri nasaha na
upimaji wa VVU vimeongezeka kutoka vituo 87 mwaka 2012 hadi kufikia vituo 91
mwaka 2015. Kati ya hivyo, Unguja 58 na Pemba 33. Vile vile, Serikali inaendelea
kuwahamasisha wananchi kuwa na tabia ya kupima afya zao na kujiepusha na
maambukizi mapya ya UKIMWI.
27.0 Mheshimiwa Spika, kwa upande wa tatizo la dawa za kulevya,
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais inasimamia utekelezaji wa
Sheria ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya Namba 12 ya mwaka 2011. Mpango Maalum
(Road Map) wa Utekelezaji wa Sheria hiyo umeandaliwa na unatekelezwa kwa
kushirikisha wadau kutoka Taasisi mbali mbali za Serikali na zisizo za Serikali
ili kuhakikisha kwamba michango mbali mbali inatolewa kudhibiti uingizaji,
usafirishaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya. Vile vile,
Serikali imeandaa Sera ya Dawa za Kulevya na kufanya mikutano na vyombo vya
kusimamia sheria (Law Enforcement Agency) ili kukuza mashirikiano na vyombo
hivyo katika kudhibiti Dawa za Kulevya.
28.0 Mheshimiwa
Spika, ujenzi wa Kituo Maalumu cha Kurekebisha Vijana walioathirika
na Dawa za Kulevya katika eneo la Kidimni, Wilaya ya Kati unaendelea. Aidha, Nyumba za Marekebisho ya Tabia (Sober
Houses) 13 zimeanzishwa ambazo zimetoa huduma kwa vijana 1,020 kwa Unguja na
Pemba. Serikali imechukua jitihada kubwa ya kuziendeleza nyumba hizo ili ziweze
kutoa huduma zinazostahiki. Serikali
kupitia Vituo vya Ushauri Nasaha imeendelea kutoa ushauri nasaha kwa waathirika
wa dawa za kulevya. Pia, taaluma juu ya athari za Dawa za Kulevya imetolewa katika Shehia
mbali mbali za Unguja na Pemba, Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
pamoja na Skuli kupitia mikutano, makongamano, semina pamoja na utoaji wa
kalenda na vipeperushi.
29.0 Mheshimiwa
Spika, Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo inaendelea
na jitihada zake za kuwapatia wananchi wake huduma bora ya maji safi na
salama. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali ya Awamu ya Saba imetekeleza
Miradi 10 na Programu mbili (2) za kuwapatia wananchi wake maji safi na
salama pamoja na kuendeleza Mpango wa Kulinda Vyanzo vya Maji Unguja na Pemba.
Vile vile, Serikali imeifanyia matengenezo makubwa miundombinu ya usambazaji
maji katika maeneo mbali mbali mjini na vijijini ili kuhakikisha
kuwa huduma ya maji inapatikana kwa wananchi wakati wote bila ya
usumbufu. Serikali imechukua hatua maalumu ya kuziondosha mita 41 za TUKUZA
zilizokuwepo katika visima mbali mbali vya miradi ya maji ili kuwaondoshea kero
wananchi na kuhakikisha wanapata huduma ya maji safi na salama bila ya
usumbufu.
30.0 Mheshimiwa
Spika, ili kuhakikisha kwamba Zanzibar inakua na umeme wa uhakika, Serikali
imesimamia kikamilifu utekelezaji wa mradi wa kujenga njia ya pili ya umeme
inayopita chini ya bahari kutoka Ras Kiromoni Tanzania Bara hadi Fumba
Unguja. Pamoja na hatua hiyo, Serikali pia imo katika juhudi ya kutafuta
miradi ya umeme mbadala, kwa kutumia ama jua, upepo au mawimbi ya baharí, hii
itategemea na utafiti unaofanywa kujua ni aina gani ya umeme unatufaa kwa
mazingira ya nchi yetu.
Aidha, kwa msaada wa Serikali ya Norway,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeunganisha umeme toka Majani Mapana, Tanga
hadi Wesha huko Pemba ili wananchi wa Pemba wapate umeme wa uhakika.
Umeme huu una nguvu ya 20MW, hadi sasa ni matumizi ya 6MW tu ndiyo
yaliyofikiwa. Waya huu unaweza kuishi kwa muda wa miaka 30 hadi 40.
Umeme huu umeanza kutumika kuanzia mwaka 2010.
31.0 Mheshimiwa
Spika, katika kuendeleza matumizi bora ya ardhi nchini (Land use
Planning), Serikali imekamilisha Mpango Mkuu wa Kitaifa wa Matumizi Bora ya
Ardhi wa Zanzibar. Utekelezaji wa Mpango huu utasaidia kupunguza matumizi
holela ya ardhi. Sambamba na Mpango huo, Serikali imetayarisha
Sheria ya kuanzisha Kamisheni ya Ardhi itakayosimamia matumizi yote ya ardhi
nchini. Aidha, Serikali imeendelea kuziimarisha mahakama za ardhi kwa kuzipatia
vitendea kazi na kuziongezea idadi ya Mahakimu. Juhudi zote hizi zimelenga
katika kupunguza tatizo la migogoro ya ardhi hapa nchini. Ni matumaini
yangu Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako watasaidia kuhakikisha kuwa migogoro
ya ardí inakuwa historia nchini mwetu.
MAMBO YALIYOJADILIWA KATIKA MKUTANO WA 20:
32.0 Mheshimiwa
Spika, Mkutano
huu wa 20 ulikuwa ni mkutano wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2015/2016 ambapo
Bajeti ya Serikali, Mpango wa Maendeleo pamoja na bajeti za Wizara zote
ziliwasilishwa, kujadiliwa na kupitishwa. Aidha, katika Mkutano huu jumla
ya maswali ya msingi 72 na maswali ya nyongeza 174 yaliulizwa na Waheshimiwa
Wajumbe na kujibiwa na Waheshimiwa Mawaziri. Pia, Mswada wa Sheria Namba
9 ya 2015 ya Kutoza Kodi na Ushuru na Kurekebisha Sheria Nyengine za Fedha na
Sheria za Kodi Zinazohusiana na Ukusanyaji na Udhibiti wa Mapato ya Serikali na
Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo, uliwasilishwa, kujadiliwa na kupitishwa na
Baraza lako Tukufu.
Vile vile, Baraza lilijadili na kupitisha
Sheria Namba 10 ya 2015 ya Kuidhinisha Makisio na Matumizi ya Shilingi Mia Nane
na Thalathini, Mia Tatu na Sitini Milioni na Laki Tatu kutoka Mfuko Mkuu wa
Hazina ya Serikali kwa mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2016 na
kuruhusu Utoaji na Uhaulishaji wa Fedha Hizo pamoja na Mambo Yanayohusiana na
Hayo.
33.0 Mheshimiwa Spika, pamoja na jukumu muhimu la Mkutano huu
la kuwasilisha, kujadili na kupitisha Bajeti ya Serikali, Mpango
wa Maendeleo pamoja na bajeti za Wizara zote, Baraza pia lilipata fursa ya
kujadili hoja mbali mbali zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wajumbe. Miongoni mwa
hoja hizo ni pamoja na hoja ya ukarabati wa nyumba za Mji Mkongwe, mapambano
dhidi ya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia, migogoro na unyanyasaji wa
wafanyakazi katika makampuni na hoja inayohusiana na malipo ya posho na stahiki
za walimu.
34.0 Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na juhudi ya kuzipatia
ufumbuzi hoja mbali mbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako
Tukufu. Suala la ukarabati wa Mji Mkongwe, Serikali tayari imeshafanya tathmini
na jumla ya nyumba 26 zimegundulikana kuwa mbovu na zinahitaji ukarabati
mkubwa. Kutokana na uwezo wa Serikali wa kuzikarabati nyumba hizo kuwa
mdogo, imeamua kuziuza baadhi ya nyumba hizo. Aidha, katika kusimamia
suala la udhalilishaji na unyanyasaji wa kijinsia, Serikali itaendeleza
mashirikiano na wananchi katika kupambana udhalilishaji wa aina zote
nchini. Hivyo, Serikali inawaomba wananchi waendeleze mashirikiano baina
yao na Serikali yao katika kuwafichua wale wote wanaofanya vitendo vya
udhalilishaji.
35.0 Mheshimiwa Spika, katika kulishughulikia tatizo la migogoro na
unyanyasaji wa wafanyakazi katika makampuni hasa ya kitalii, Serikali kupitia
Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma inaendelea kuwakumbusha
wamiliki wa mahoteli kufuata kanuni na sheria za kazi zilizopo nchini na
kuwacha kuwanyanyasa wafanyakazi wao. Aidha, Serikali inawataka waajiriwa wa
makampuni hayo kuwasilisha malalamiko yao Wizarani ili Wizara ichukuwe hatua
zinazofaa. Vile vile, kwa upande wa malipo ya stahiki na maposho kwa
walimu waliosimamia mitihani iliyopita, Serikali tayari imeshalipa stahiki na
maposho kwa baadhi ya walimu na hatua za kuwakamilishia stahiki na maposho kwa
walimu waliobakia zinaendelea.
36.0 Mheshimiwa
Spika, harakati za Uchaguzi Mkuu wa 2015 tayari zimeanza kwa
Vyama vya Siasa kutafuta wagombea wa nafasi mbali mbali za uongozi wa nchi
yetu. Ni muhimu kwetu sisi viongozi kuzidi kuwanasihi wafuasi wetu na
wananchi kwa ujumla kujiepusha na aina zote za vitendo vitavyoweza kupelekea
uvunjifu wa amani na usalama wa nchi yetu. Ni imani yangu kwamba, tunaweza
kuchaguana bila ya kutukanana, kugombana, kuchukiana, kuhasimiana au kufanya
vurugu za aina yoyote ile. Hii ni nchi yetu sote na hivyo, usalama
na amani ni muhimu kwetu sote. Mafanikio yetu tuliyoyapata kwa muda mrefu
na maendeleo yetu yanategemea kudumu kwa hali ya amani na utulivu katika nchi
yetu. Nawasihi wananchi wote watumie haki yao ya kidemokrasia kuchagua viongozi
makini wenye nia ya dhati na uwezo wa kuwatumikia na kuwaletea maendeleo
wananchi. Serikali itahakikisha ulinzi na usalama unaimarika na haitokuwa
tayari kumvumilia mtu yeyote au kikundi chochote kitakachovunja sheria na
kuhatarisha amani na utulivu wa nchi yetu. Tusifikirie hata siku moja
kuwa vikundi vinavyojitayarisha au kutayarishwa kufanya vitendo vya kuhatarisha
amani ya nchi kuwa vinaikomoa Serikali bali vinajikomoa vyenyewe.
Tunawaomba wazazi kuwadhibiti vijana wao ili wasijiingize katika vitendo vya
uvunjifu wa amani.
37.0 Mheshimiwa
Spika, kabla ya kumalizia hotuba yangu, naomba kwa mara nyengine tena
nikushukuru wewe binafsi kwa jinsi ulivyoliendesha Baraza kwa umakini na
uadilifu mkubwa. Narudia kuwashukuru pia, Mheshimiwa Naibu Spika, Wenyeviti wa
Baraza na Wenyeviti wa Kamati za Kudumu kwa kutekeleza majukumu yao vyema
katika kipindi chote cha miaka mitano (5). Vile vile, nawashukuru Waheshimiwa
Mawaziri, Naibu Mawaziri, Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi,
Makatibu Wakuu wa Wizara zote na Watendaji wote wa Serikali kwa utendaji wao
mzuri uliotuletea mafanikio makubwa katika nchi yetu.
38.0 Mheshimiwa
Spika, kwa aina ya pekee namshukuru Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais, Mheshimiwa Mohamed Aboud Mohamed, Katibu Mkuu na Naibu Katibu
Mkuu, Afisa Mdhamini, Wakurugenzi na Watendaji wote wa Ofisi yangu kwa namna
walivyonipa mashirikiano na kunisaidia katika kutekeleza majukumu yangu.
Aidha, napenda kuwashukuru wake zangu Bi. Pili Juma Iddi na Bi. Asha Suleiman
Iddi na familia zangu kwa ujumla kwa namna walivyonipa moyo, kunivumilia na
kunisaidia katika kipindi chote nilichotumikia nchi yetu katika nafasi hii ya
Makamu wa Pili wa Rais. Zaidi namshukuru sana Bi. Asha kwa namna
alivyonisaidia katika shughuli za Jimbo langu la Kitope wakati nikiwa na shughuli
nyingine za Kitaifa. Pia, napenda kuwashukuru sana wananchi wangu wa
Jimbo la Kitope kwa kushirikiana nami katika kipindi chote cha miaka mitano kwa
nia ya kuliletea Jimbo letu maendeleo. Nawaomba waniunge tena mkono
nitakapokwenda kuomba ridhaa yao ya kuwatumikia.
39.0 Mheshimiwa
Spika, navishukuru vyombo vyote vya habari vilivyoshirikiana nasi
katika Baraza hili wakiwemo wataalamu wetu wanaotafsiri kwa lugha ya
alama waliowawezesha wenzetu wenye matatizo ya kusikia kufuatilia mijadala na
shughuli mbali mbali za Baraza. Pia, namshukuru Katibu wa Baraza la Wawakilishi
na wafanyakazi wote wa Baraza hili kwa maandalizi mazuri ya mikutano
yote. Kwa aina yake napenda kumshukuru sana Mhasibu wa Baraza kwa kazi
nzuri alizofanya katika kipindi chote cha miaka mitano kuwahudumia vizuri
Wajumbe wa Baraza.
40.0 Mheshimiwa
Spika, nawatakia kila la kheri Waheshimiwa Wajumbe
wa Baraza lako Tukufu watakaopata nafasi ya kurudi Majimboni kuomba
ridhaa ya wananchi kuchaguliwa tena kuingia Baraza líjalo. Nawatakia
kheri katika mchakato huo na ni matumaini yangu kwamba wengi wetu tutarudi tena
katika Baraza hili kuendelea kuwatumikia wananchi. Lakini pia
nawatakia kila la kheri wale Wajumbe ambao hawatopata bahati ya kurudi tena
Barazani hapa, nawaombea wafanikiwe katika mambo watakayoamua kuyafanya hapo
baadae.
41.0 Mheshimiwa
Spika, mwisho napenda kuchukua nafasi hii kuelezea masikitiko yangu
kwa lile jambo lililotokea Barazani huku tarehe 23 Juni, 2015 kwa Mawaziri na
Wajumbe wengine wa Baraza lako tukufu kutoka Chama cha CUF kuamua kutoka nje ya
Baraza wakati Baraza lilipotaka kupitisha sheria ya matumizi kutokana na Bajeti
zilizowasilishwa Barazani. Kitendo hiki hakikuwatendea haki wananchi
kwani kama sheria ya matumizi isingepita maana yake Serikali ingeshindwa
kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo kwa vile isingekuwa na fedha.
42.0 Mheshimiwa
Spika, napenda kuwapongeza kwa dhati Waheshimiwa Mawaziri na Wajumbe
wengine wa Baraza lako tukufu kutoka Chama cha Mapinduzi kwa kuchukua hatua
madhubuti kuhakikisha kuwa sheria ya matumizi inapita. Kitendo hicho
kilikuwa cha kizalendo na kimeonyesha upendo kwa wananchi wetu. Hongereni
sana.
43.0 Mheshimiwa
Spika, kwa
vile Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali
Mohamed Shein leo tarehe 26 Juni, 2015 saa 9.30 jioni atakuja kulihutubia Baraza
hili na baadae kutoa tamko la kulivunja, sasa kwa ruhusa yako naomba kutoa hoja
ya kuliakhirisha Baraza lako Tukufu hadi hapo saa 9.30 barabara za jioni.
44.0 Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa hoja.
0 comments:
Post a Comment